Simeone awataka vijana wake ‘kukomaa’

MADRID:KOCHA mkuu wa Atletico Madrid Diego Simeone amewaasa wachezaji wake ‘kushikilia bomba’ mpaka mwisho wa msimu baada ya hapo jana kikosi chake kuichabanga Rayo Vallecano mabao 3-0 na kuendelea kuikamatilia kwa nguvu nafasi ya 3 kwenye msimamo wa LaLiga.
Akizungumza na waandishi wa Habari baada ya mchezo huo Simeone amesema kwa sasa wachezaji wake wanamuelewa na wanafunga magoli lakini amewataka kujiandaa na hali ya mchezo wa soka ambao mara zote hautabiriki na umekuwa wa kubadilika badilika hivyo waendelee kuipambania timu.
“Hainikasirishi kwa kuwa kwa sasa tunafunga magoli, bado tupo kwenye mchakato. Mchezo wa mpira wa miguu una mambo mengi yasiyotabirika na lazima tujiandae kwa kila litakalokuja. Tumekuwa washindani wazuri kwenye ligi natumai hili litaendelea kwa kila mechi mpaka mwisho wa msimu” – amesema
Atletico wapo nafasi ya 3 kwenye msimamo wa LaLiga wakiwa na pointi zao 66 baada ya ushindi wa jana katika dimba lao nyumbani la Riyadh Air Metropolitano wakiwa pointi 10 nyuma ya vinara FC Barcelona na pointi sita nyuma ya Real Madrid wanaoshikilia nafasi ya pili
Simeone amekubali kuwa ubingwa ligi hiyo unabaki ndoto tu kwa sasa akisisitiza ulinzi zaidi wa nafasi hiyo ambayo inawapa kiti kweye Ligi Ya Mabingwa Barani Ulaya msimu ujao, nafasi ambayo Simeone anaamini itapotea ikiwa hawatailinda.