Featured

Simba yaweka mikakati kuimaliza Galaxy

UONGOZI wa klabu ya Simba na wakuu wa benchi la ufundi wa timu hiyo wamefanya kikao kizito usiku wa kuamkia jana kupanga mikakati ya kuwakabili wapinzani wao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika,  Jwaneng Galaxy  ya Botswana.

Simba iliyotolewa hatua ya robo fainali ya michuano hiyo msimu uliopita, imepangwa kuanzia ugenini dhidi ya  mabingwa hao wa Botswana.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wao mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ ambapo moja ya mikakati yake kuelekea kuanza michuano hiyo alitaka kuona Simba inapata ushindi na kutinga hatua ya makundi.

“Tulikuwa na kikao na viongozi wetu wa juu, suala la msingi ilikua ni kujadili na kupanga mikakati ya kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mchezo wetu wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika na wenzetu wametuahidi kutupa kila sapoti ili kuhakikisha tunafanya vizuri kama ambavyo tumekusudia,” alisema Rweyemamu.

Meneja huyo alisema maandalizi yao kuelekea mchezo huo yanakwenda vizuri na wachezaji  wote wapo katika hali nzuri wakiwemo waliokuwa kwenye timu za taifa tayari wameungana na wenzao kambini.

Alisema kwake matumaini ya kufanya vizuri na kufika mbali kwenye michuano hiyo ni makubwa  kutokana na utayari wa wachezaji  baada ya kufanya mazoezi na kucheza mechi kadhaa za kirafiki ambazo ana amini zimezidi kuwaimarisha na kumaliza makosa yaliyojitokeza katika baadhi ya mechi zao.

“Tupo tayari kwa ajili ya michuano hiyo, maandalizi yetu yanakwenda vizuri, nafurahi kuona hata wachezaji wetu waliokuwa majeruhi kama Shomari Kapombe, Erasto Nyoni na Papy Sakho wote wamepona na wameshaanza mazoezi na wenzao,” alisema.

Simba ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya Yanga kutolewa mapema na timu ya Rivers United ya Nigeria mwezi uliopita.

Related Articles

Back to top button