Simba, Yanga zatozwa faini

DAR ES SALAAM: KLABU ya Simba imetozwa faini ya jumla Sh milioni 20 na Yanga Sh milioni tano kutokana na makosa tofauti katika mechi mbili tofauti ikiongozwa na Dabi iliyochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar.
Simba ilitozwa sh milioni tano kwa kosa la kuingia kwenye uwanja wa Amaan, Zanzibar kupitia mlango usio rasmi kuelekea mchezo tajwa hapo juu kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:21 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa ligi iliyotolewa leo, Klabu ya Simba pia, imetozwa faini ya milioni tano kwa kosa la kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye uwanja wa Amaan, ambapo walitumia chumba cha kufanyia mikutano ya Wanahabari kwa shughuli hiyo kabla ya kuanza mchezo,.
Simba na Yanga kila mmoja ametozwa sh milioni tano kwa kosa la walinzi wake kugombana na kutoleana lugha ya matusi, jambo lililozua taharuki na kuchafua taswira ya mchezo huo wakati klabu ya Simba ikiwasili uwanjani hapo.
Klabu ya Simba italazimika kulipa gharama za matengenezo ya mlango wa kuingilia chumba cha kufanyia mikutano ya Wanahabari ambao walinzi wake waliuvunja ili kulazimisha timu hiyo kuingia na kutumia chumba hicho kwa ajili ya kuvalia kabla ya kuanza kwa mchezo huo.
Mbali na mchezo huo wa Dabi, Simba imetozwa faini ya Sh. Milioni tano kwa kosa la mashabiki wake kumrushia chupa za maji mchezaji William Edgar wa Dodoma Jiji wakati akitoka kiwanjani katika mchezo kati ya Dodoma Jiji na Simba pamoja na kuwarushia chupa watoa huduma ya kwanza (Redcross) wakati wakitekeleza majukumu yao kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Adhabu hiyo imetolewa pia, kwa Klabu ya Dodoma Jiji kwa kosa la maofisa wake wa huduma ya kwanza (Redcross), kuonekana mara kadhaa wakichelewa kwa makusudi kuingia kiwanjani pale walipotakiwa kufanya hivyo na mwamuzi wa mchezo huo, hali iliyotafsiriwa kama hila ya kupoteza muda.
Mchezaji David Kameta wa klabu ya Simba ametozwa faini ya Sh. milioni moja kwa kosa la kuonekana akimwaga kimiminika kiwanjani wakati timu hiyo ilipozuru uwanja dakika chache baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Amaan, kitendo kilichotafsiriwa kama Imani za kishirikina.




