Simba Queens kufa au kupona


FAINALI ya Samia Cecafa Cup inatarajia kuchezwa leo, ambapo Simba Queens itaikabili She
Corporate ya Uganda katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti la HabriLEO kocha wa Simba Queens, Sebastian Nkoma amesema wachezaji wana ari ya kuandika historia ya kuwa mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Kanda ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
“Tumejiandaa vema na wachezaji wana ari, hatuwezi kuwadharau wapinzani wetu, tutaingia kwa kuwaheshimu maana hadi wanafika fainali inamaanisha ni timu bora,” amesema Nkoma.
Simba Queens katika mchezo wa nusu fainali waliifunga AS Kigali WFC mabao 5-1 na She Corporates waliifunga CBE ya Ethiopia kwa mabao 2-1.
She Corporates walikuwa Kundi B na Simba Queens na waliifunga mabao 2-0 katika hatua ya makundi.
Mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu utakuwa dhidi ya AS Kigali na Commercial Bank FC.
Michuano hiyo ambayo inadhaminiwa na Rais Samia Suluhu Hasaan ‘Samia Cecafa Cup’ ilianza Agosti 15 ikichezwa katika makundi mawili.
Kundi A, Commercial Bank FC ya Ethiopia, AS Kigali ya Rwanda, Fofila PF ya Burundi na Warriors Queens ya Zanzibar wakati Kundi B lilikuwa na timu za Simba Queens, She Corporate ya Uganda, Yei Joints Stars ya Sudan Kusini na Garde Republicane ya Djibouti.
Mbali na zawadi za Dola za Marekani 30,000 (sawa na Sh milioni 70), pia bingwa ataziwakilisha nchi za Cecafa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Zawadi hizo hutolewa na Rais Samia na mshindi wa pili atapata Dola za Marekani 20,000 (sawa na Sh milioni 47) na mshindi wa tatu atapewa Dola za Marekani 10,000 (sawa na Sh
milioni 23,3).