Simba kwenda Sudan Agosti 26

KIKOSI cha Simba kimeingia kambini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana utakaofanyika Agosti 28 kwenye Uwanja wa Omdurman nchini Sudan.
Simba inayoongoza Ligi Kuu Bara baada ya michezo miwili itakwenda Sudan ikiwa timu mwalikwa katika mashindano maalumu yaliyoandaliwa na klabu ya Al Hilal FC yakiwa ni maandalizi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wekundu wa Msimbazi wanatarajiwa kuondoka Agosti 26 kwenda Sudan kushiriki mashindano hayo yatakayoshirikisha timu tatu ambazo ni wenyeji Al Hilal na Asante Kotoko kutoka nchini Ghana.
Akizungumza na gazeti la HabariLEO, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally, amesema kuwa
wanaenda Sudan na wachezaji wao wote isipokuwa tisa ambao wako kwenye kambi ya timu ya taifa ya Tanzania inayojiandaa na mchezo wa kufuzu mashindano ya Chan dhidi ya Uganda.
“Kikosi chetu kiko kamili baada ya michezo miwili ya ligi hatujapata majeruhi hivyo
wachezaji wote wako fiti na tunatarajiwa kuondoka na kikosi chote kwenda nchini Sudan,
tayari wachezaji wote hivi sasa wako kambini,” alisema.
Katika hatua nyingine, Ally amesema kuwa baada ya kuwa na malalamiko kuhusu suala la
uchache wa jezi mzabuni aliahidi kuwa jana Jumatano tatizo hilo lingekuwa limefanyiwa kazi, hivyo wanapaswa kuwa na subira wakati suala hilo linashughulikiwa.