Ligi Kuu

Simba kurejea kibaruani kesho

DAR ES SALAAM: WEKUNDU wa Msimbazi Simba wanatarajia kurejea Ligi Kuu kesho watakapovaana na wenyeji KMC kwenye Uwanja wa KMC Complex Dar es Salaam.

Morali ya Simba katika mchezo huo iko juu hasa baada ya kutoka kuonesha kiwango bora ugenini katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Atletico ya Angola walikotoka sare ya bao 1-1.

Kupitia mchezo huo, wachezaji wapya wa Simba waliosajiliwa kwenye dirisha dogo walionesha kiwango kizuri na matumaini kwa wekundu hao wakiamini sasa wanarudisha majeshi yao nyumbani na kipaumbele chao ni kufanya vizuri katika michezo ya Ligi Kuu.

Simba iliyopo katika nafasi ya saba imeshacheza michezo saba ikiwa na viporo vya michezo zaidi ya sita. Timu hiyo imevuna pointi 16 baada ya kushinda michezo mitano, sare moja na kupoteza mchezo mmoja.

Inakutana na KMC ambayo, imetoka kupoteza mchezo uliopita wa Ligi Kuu kwa mabao 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji na kuendelea kushika mkia kwa point inane katika michezo 14 waliyocheza.

Simba kama ilivyo kwa KMC wote wanahitaji ushindi kujiweka katika nafasi nzuri ingawa kiufundi wekundu hao wako vizuri kuliko KMC.

Kocha wa Simba Steven Barker amesema maandalizi yanakwenda vizuri na kwamba wanahitaji kucheza mechi hiyo vizuri ikiwemo kutawala mchezo na kupata ushindi.

Mchezo mwingine, Singida Black Stars watacheza na Fountain Gate katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Singida wametoka kupoteza mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CR Belouzdad ya Algeria kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex. Fountain imetoka kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Namungo kwenye mchezo wa Ligi Kuu.

Kila mmoja anahitaji ushindi kujiweka sehemu nzuri kwenye ligi.

Related Articles

Back to top button