
MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu amesema klabu hiyo italitumia dirisha dogo Januari 2023 kukiimarisha kikosi ili kufanya vizuri kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza na SpotiLeo leo Mangungu amesema mpango huo ni kusajili wachezaji wawili hadi watatu na hiyo inatokana na maelekezo kutoka kwa mkuu wa benchi la ufundi Juma Mgunda.
“Tumepanga kuimarisha safu yetu ya ushambuliaji tutaongeza mshambuliaji mmoja ili akasaidiane na washambuliaji waliopo lakini pia tutasajili beki mmoja wa kati na kiungo wa juu kwa ajili ya kutengeneza mashambulizi,” amesema Mangungu.
Amesema mbali na kusajili wachezaji pia suala lingine linalopewa uzito ni kuliongezea nguvu benchi la ufundi ili kusaidiana na kocha Juma Mgunda baada ya msaidizi wake Seleman Matola kwenda masomoni.
Mangungu amesema mchakato wa kusajili wachezaji wanaokusudiwa unakwenda vizuri na kuhusu suala la kocha klabu inakamilisha taratibu za mwisho kabla ya kumtangaza kocha mpya.
Wiki iliyopita Bodi ya Wakurugezi wa Simba ilikutana kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya timu hiyo na miongoni mwa yaliyopewa kipaumbele ni maboresho ya kikosi cha timu ya wanaume.