Ligi Daraja La Kwanza

Simba, B19 mchezo wa jasho na heshima

DAR ES SALAAM: WEKUNDU wa Msimbazi Simba kesho Jumamosi watashuka dimbani kuikaribisha timu ya Championship ya B19 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB utakaochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Dar es Salaam.

Kuelekea katika mchezo huo wa mtoano hatua ya 32 bora, Kocha Mkuu wa Simba Steven Barker amesema anaamini utakuwa mchezo wenye ushindani hivyo, wamejipanga vizuri kupambana na kushinda.

Barker amekoshwa na kiwango bora kilichooneshwa na wachezaji wake kwenye mazoezi akisema ni wa hali ya juu.
“Namna mnavyocheza kwa nguvu, kwa ari na kwa ushindani imenivutia sana. Nimefurahishwa kwa kiwango hiki cha juu, hongereni kwa kazi nzuri. Nawatakieni kila la heri mnapoendelea mbele.”amesema.

B19 inakwenda kukutana na Simba ambao wako kwenye morali na wametoka kuonesha soka la kuvutia katika mchezo wa dabi dhidi ya Yanga licha ya kupata sare tasa watataka kuendelea kuonesha kuwa hawakubahatisha.

Kiufundi Simba ni bora katika safu ya ushambuliaji n ahata ulinzi na takwimu zake ligi zinaonesha hivyo, wakiwa katika nafasi ya tatu, kwa pointi 24 ndani ya michezo 11, wakiwa wamefunga mabao 18 na kufungwa manne.

B19 licha ya kwamba inashiriki ligi ya championship bado haipaswi kubezwa na mara nyingi timu ndogo zimekuwa zikitaka kuonesha soka zuri kama sehemu ya wao kujiuza na wachezaji wanajua wazi ni sehemu ya kuonekana kwao, ni lazima watajitahidi kuonesha kiwango.

Timu hiyo ya Championship imetengewa fungu la mamilioni na uongozi wake kama motisha kuhakikisha wanaitoa Simba. Huenda ukawa mchezo wa jasho kwa Simba ambao wanataka kuvuka na B19 kutengeneza historia yao mpya ya kuwaondosha wekundu hao. Dakika 90 zitaamua.

Related Articles

Back to top button