Nyumbani

Shime: Mvua ilituvuruga lakini tulivuka

EQUATORIAL GUINEA: KOCHA  Mkuu wa Twiga Stars, Bakari Shime, amesema mvua kubwa iliyonyesha wakati wa mechi yao ya marudiano dhidi ya Equatorial Guinea iliathiri mbinu zao za mchezo katika harakati za kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026.

Twiga Stars walilazimisha sare ya 1-1 baada ya kusawazisha bao katika kipindi cha pili kwenye mchezo uliochezwa jana nchini humo. Matokeo hayo yaliwafanya kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-2.

Shime amesema kuwa mechi hiyo ilikuwa ngumu, hasa kutokana na hali mbaya ya hewa.

“Mvua kubwa ilianza kunyesha ghafla, uwanja ukawa unateleza, na tukalazimika kubadilisha mbinu zetu za kawaida za mchezo. Wapinzani walicheza mipira mirefu, na kwa bahati mbaya, tumekumbana na idadi kubwa ya faulo na mipira ya adhabu (free kicks) kuliko kawaida,” amesema Shime.

Hata hivyo, kocha huyo alisifu wachezaji wake kwa uimara wao, akisema kuwa walifanikiwa kurekebisha makosa yao baada ya kipindi cha kwanza kigumu.

“Kipindi cha kwanza hali ya hewa ilikuwa changamoto kwetu, lakini katika mapumziko niliwapa maelekezo sahihi, na tukaweza kusawazisha bao na kusonga mbele,” ameongeza.

Twiga Stars sasa inajiandaa kwa raundi ya pili ya michuano hiyo, ambapo watakutana na Ethiopia.

Related Articles

Back to top button