Kwingineko

Serie A kurejea na kishindo cha Milan Derby

MILAN: JUMAPILI usiku jiji la Milan litakuwa kitovu cha burudani wakati mahasimu wa jiji hilo, Inter Milan na AC Milan, watakapokutana San Siro katika pambano linaloamua kilele cha Serie A, huku Napoli wakijaribu kurejea kwenye reli baada ya mapumziko ya kimataifa.

Inter ndio wanaoongoza ligi kwa tofauti ya mabao dhidi ya Roma, na wanarejea katika uwanja wa San Siro baada ya timu ya taifa kushindwa vibaya dhidi ya Norway wiki iliyopita. Kikosi cha Cristian Chivu kipo kileleni kikiwa pointi mbili mbele ya AC Milan, ambao wanakamata nafasi ya tatu nyuma ya Roma.

Inter wapo kwenye kiwango cha juu wameshinda mechi 11 kati ya 12 walizocheza hivi karibuni katika mmashindano yote, kichapo chao pekee kikiwa ni kile cha Napoli mwezi uliopita huku wakiwa kwenye mbio za kuwania Scudeto

Baada ya derby, Inter wataelekea Madrid kuivaa Atletico wakiwa na matumaini ya kusogea hatua moja kuelekea 16 bora ya Champions League baada ya kushinda mechi zote nne za Ulaya mpaka sasa.

Marcus Thuram anaweza kuanza kwa mara ya kwanza tangu Septemba baada ya kupona jeraha la msuli wa paja lililomkosesha mechi za kufuzu Kombe la Dunia na Ufaransa. Hata hivyo, Denzel Dumfries anatarajiwa kukosa mechi ya Jumapili kutokana na jeraha la kifundo cha mguu, na Carlos Augusto huenda akabadilishwa upande ili kutoa upana kwenye uwanja.

Kwa upande mwingine, AC Milan wanapata habari njema za kurejea kwa Adrien Rabiot ambaye alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya paja aliyopata akiwa na Ufaransa mwezi uliopita. Kocha Massimiliano Allegri anatarajia Rabiot pamoja na Luka Modric watacheza derby yao ya kwanza ya jiji la Milan.

Napoli bado wanapigania ubingwa lakini upepo ndani ya klabu ni mzito. Wakiwa na pointi sawa na Milan (22), mabingwa hao watetezi wanakabiliwa na presha baada ya Antonio Conte kulipuka kwa hasira kufuatia kichapo cha 2-0 dhidi ya Bologna. Maneno yake makali akidai hawezi kusindikiza wafu yamezua tetesi za kujiuzulu. Conte alipewa siku chache kupoa wakati wa mapumziko ya kimataifa.

Lakini matatizo hayajaisha. Kiungo muhimu Andre-Frank Anguissa ameumia akiwa na Cameroon na atakosa mechi mpaka mwakani, jambo ambalo limemkasirisha sana rais wa Napoli, Aurelio De Laurentiis, ambaye sasa anataka fidia kwa wachezaji wanaoumia wakiwa kwenye majukumu ya taifa.

Jumamosi, Juventus ya Luciano Spalletti inarejea kwa matumaini mapya dhidi ya Fiorentina, ambao wanasuasua na kukamata mkia wa ligi. Spalletti anarudi katika mkoa wake wa nyumbani, Tuscany, ambako safari yake ya ukocha ilianza zaidi ya miaka 30 iliyopita. Kwa Fiorentina, huu ni mchezo muhimu chini ya kocha mpya Paolo Vanoli ambaye anatafuta njia ya kuokoa msimu wao.

Related Articles

Back to top button