
DAR ES SALAAM:KATIBU Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Kedmon Mapana, amesema kuwa sekta ya sherehe imekua kwa kasi na sasa inatambuliwa rasmi kama sehemu muhimu ya tasnia ya sanaa nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tuzo za Tanzania Event Planners Awards, Mapana alieleza kuwa mfumo mpya uliozinduliwa na Baraza utasaidia kufuatilia idadi ya wanaofanya kazi katika sekta hiyo pamoja na mapato yao ya kila mwezi na mwaka.
“Mkisema mnalipa kodi kubwa, lazima tuwe na takwimu sahihi – mnajua ni wangapi na mnapata kiasi gani? Mfumo huu utatusaidia kuwatambua, na mwakani BASATA tutakuwa na data kamili ili kuwaombea TRA kuwapunguzia kodi kulingana na mchango wenu,” alisema Mapana.
Alisisitiza kuwa kila msanii au mtoa huduma katika sekta ya sanaa anatakiwa kujisajili na kuwa na kitambulisho cha NIDA ili kuwezesha ufuatiliaji sahihi wa mapato na idadi ya wasanii.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Sanaa za Maonesho, Sintia Enjewele, alimpongeza Mapana kwa mchango mkubwa katika mageuzi ya sekta ya sanaa tangu alipokabidhiwa jukumu la kuongoza BASATA.
Katika hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, alitunukiwa tuzo ya Kiongozi Bora kwa mchango wake mkubwa katika kuendeleza sekta ya sanaa nchini.
Tuzo nyingine zilikwenda kwa Katibu wa BASATA kwa kuleta mapinduzi katika tasnia ya muziki na burudani, ikiwa ni ishara ya kutambua juhudi za kuboresha sekta hiyo.