Nyumbani

SAMIA na dhamira ya mapinduzi kwenye michezo

JUMATATU ya Juni 5 itabaki kwenye kumbukumbu za timu ya Yanga, baada ya kualikwa Ikulu na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuwapongeza kwa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga imekuwa timu ya kwanza kutoka nchini Tanzania na ukanda wa Cecafa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho, ambalo lilipatikana baada ya kuunganisha Kombe la Washindi na Kombe la Caf mwaka 2004.

Hata hivyo, Simba ndio ilikuwa ya kwanza kwa timu za Tanzania kucheza fainali za Afrika baada ya mwaka 1993 kucheza fainali ya Kombe la Caf na kutolewa na Stella Abidjan kwa kufungwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru).

Lakini pia Yanga ndio klabu iliyocheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mara nyingi zaidi kwa timu za hapa nchini ikifanya hivyo mwaka 2016, 2018 na 2023.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema kuwa wakati anaingia madarakani alijisemea kuwa anataka kurejesha heshima kwenye michezo, kitu ambacho kimeanza kuonekana.

Awamu ya sita chini ya Rais Samia michezo mbalimbali imepaa kwa ubora kwa mara ya kwanza timu ya taifa ya wasichana chini ya miaka 17 ilishiriki fainali za Kombe la Dunia nchini India mwaka 2022 na kuishia hatua ya nusu fainali.

Kwenye mchezo wa riadha, medali kadhaa zimekusanywa ikiwemo ya Boston Marathon ya kilometa 42, ambapo Gabriel Geay, akishika nafasi ya pili nyuma ya Evans Chebet.

Pia katika riadha Tanzania imepata medali katika Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Birmingham, Uingereza mwaka 2022 kutoka kwa Alphonce Simbu (riadha) na Yusuf Lucasi Changalawe na Kassim Mbundwike (ndondi).

Kwa miaka mingi Tanzania ilikuwa haijapata medali ya riadha katika Michezo ya Jumuiya ya Madola sambamba na ndondi ambayo kwa mara ya mwisho ilitwaa medali mwaka 1998.
Ni takribani miaka 24 ilipita kabla ya Tanzania kupata medali nyingine kutoka katika michezo hiyo ya pili kwa ukubwa inayoshirikisha michezo mingi kwa pamoja baada ya ile ya Olimpiki.

Katika ndondi za kulipwa, bondia Twaha Kassim ameshinda mkanda na Alex Kabangu, alishinda Mkanda wa UBO naye Seleman Kidunda akimpiga Tshimanga Katompa na kushinda mkanda wa WBF Intercontinental huku Karim Mandonga akishinda ubingwa wa
PST baada ya kumchapa kwa pointi Kenneth Lukyamuzi kutoka Uganda.

HISTORIA MPYA
Medali ya kwanza ya mashindano ya Caf ililetwa na timu ya Simba mwaka 1993 baada ya kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Stella Abidjan ya Ivory Coast. Wakati Yanga imekuwa
timu ya kwanza kuleta medali ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kuondolewa kwa yale ya Kombe la Caf na Kombe la Washindi.

“Yanga imeleta heshima kubwa na kuirejesha nchi kwenye ramani ya soka, wakati naingia madarakani nilisema nataka kurejesha heshima kwenye michezo yote. “Haikuwa rahisi timu
nyingi kutoka mataifa mbalimbali zilishiriki lakini Yanga imeandika historia ya kucheza fainali, wachezaji waliofanikisha hili naomba muwape heshima yao kwa  kuboresha maslahi yao kwani Chanda chema huvishwa pete,” anasema Rais Samia.

UTAIFA KWANZA
Ilikuwa imezoeleka kuona timu za Simba na Yanga zikiwapa sapoti wageni wanaokuja kucheza michezo ya mashindano ya Caf jambo ambalo Rais Samia amelikemea. Anasema anataka kutia mkazo kuwa timu yoyote itakayokuwa ikiiwakilisha nchi hiyo ni timu ya Tanzania hivyo utani wa jadi uwe nyumbani.

“Ikifanya vizuri Simba au Yanga iungwe mkono mwisho wa mashindano inatangazwa nchi utaifa uwe mbele nje tuwe kitu kimoja.”

KUANDAA AFCON 2027
Tanzania imewahi kuandaa fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 mwaka 2019 ambapo timu ya taifa ya Cameroon ilitwaa taji hilo. Mashindano ambayo yalichezwa
kwenye viwanja vya Benjamin Mkapa na Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Awamu ya sita chini ya Rais Samia, Tanzania pamoja na nchi za Uganda na Kenya zimeungana ili kuomba kuandaa fainali za Afcon 2027.

“Tumedhamiria kuwa wenyeji wa mashindano ya Afcon mwaka 2027 kwa kushirikiana na nchi za Kenya na Uganda tukipata itakuwa mashindano ya Afrika Mashariki hivyo tunatarajia kufanya ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Benjamin Mkapa pamoja na maboresho ya Uwanja wa Amaan.

“Ukiitazama 2027 sio mbali, jitihada zinapaswa zianze sasa kwani mashindano haya yataongeza chachu na kutangaza utalii wetu,” anasema Rais Samia.

KUSAPOTI VIPAJI
Anasema amekuwa akifuatilia mashindano ya Ndondo Cup na Yamle Yamle ambayo
yamekuwa yakiibua vipaji vingi ambavyo vimekuwa vikilisha timu kubwa.

“Nataka niwaambie waandaaji wa mashindano haya niko pamoja nao nitawashika mkono ili muendelee kusonga mbele, mimi kama mama nina dhima ya kulea vipaji nawaomba
wadau wajitokeze kuunga mkono juhudi.”

Michuano ya Ndondo Cup imetoa baadhi ya mastaa wanaofanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara na timu ya taifa ikiwamo Idd Seleman ‘Nado’ , Roland Msonjo, Ally Ramadhan ‘Oviedo’ hawa ni baadhi ya nyota waliopita kwenye mashindano haya.

UJENZI WA VIWANJA
Serikali ya Awamu ya 6 chini ya Rais Samia inatarajia kuanza ujenzi wa uwanja wa
michezo ya ndani yaani Arena eneo la Tanganyika Packers Kawe utakaogharimu kiasi cha Sh bilioni 200.

Uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 16,000-20,000 ambao ujenzi wake tayari unaendelea ili kuongeza fursa kwa vijana wenye vipaji kuonesha vipawa vyao.
Lakini pia Arena kama hiyo inatarajia kujengwa jijini Dodoma pia.

SHULE ZA MICHEZO
Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya michezo katika shule teule 56 nchini ikiwa ni wastani wa shule mbili kwa kila mkoa. Utekelezaji wa mradi huu kwa Mkoa wa Tabora tayari umeanza katika baadhi ya shule.

Pamoja na ujenzi wa viwanja, serikali itajenga kumbi kubwa katika shule hizo zitakazotumika kwa kazi za sanaa na michezo ya ndani pamoja na kuajiri walimu wa michezo ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/22 walimu wa michezo 83 waliajiriwa.

USHAURI WAKE
Siku maalumu ya kusherehekea mafanikio ya Yanga na kupitia mashindano haya mmeona madhaifu yenu mkayafanyie kazi ili mtimize ndoto ya Ali Kamwe ya kuning’iniza kombe na
kupita mitaa maarufu ya Kariakoo.

Msimu wa 2023/24 Tanzania itawakilishwa na timu nne katika mashindano ya Caf, ambapo kwenye Ligi ya Mabingwa, Yanga na Simba zitaipeperusha bendera ya nchi na kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Azam na Singida Big Stars zitaiwakilisha nchi.

Rais Samia amezitaka timu hizo kujifunza kupitia kwa Yanga ambayo imekuwa timu ya kwanza kufika fainali hivyo zinapaswa kufuata mkondo huo na kulileta taji la Caf hapa nchini.

Related Articles

Back to top button