Muziki

Rose Muhando, Shusho, Bukuku watunukiwa PIMEA

DAR ES SALAAM: MASTAA wa muziki wa Injili nchini Rose Muhando, Christina Shusho na Bahati Bukuku wamepokea tuzo za heshima kupitia hafla ya The Pinnacle of Mentorship & Excellence Awards (PIMEA) iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo ya kipekee ilifanyika katika Makumbusho ya Taifa, Posta, ambapo zaidi ya wanawake 15 waliotukuka katika huduma ya kiroho walitambuliwa kwa kazi zao kubwa katika jamii. Mkurugenzi na mbeba maono wa tuzo hizo, Dk Christine Mbelwa, alieleza kuwa lengo kuu la PIMEA ni kuthamini na kutambua mchango wa wanawake waliotoa maisha yao kwa ajili ya huduma ya Injili.

“Wanawake hawa wamevumilia, wamehudumu kwa moyo na kazi yao imeigusa jamii kwa kiwango kikubwa,” amesema Dk Christine kwa msisimko mkubwa. “Tunataka kizazi kijacho kijifunze kuwa kuna wanawake waliotoa maisha yao kwa ajili ya huduma.”

Mbali na Rose Muhando, Shusho na Bukuku, waliotunukiwa pia walikuwa ni Upendo Nkone, Stella Joel Frank, Mama Imelda Maboya, pamoja na viongozi wa kiroho kama Askofu Tupilike Hans, Askofu Jane Muhegi, Dk Jennifer Mgendi, Dk Anny Fernandes, na Dk Gwantwa Mwakibolwa.

Tukio hilo lilihudhuriwa na wake wa wachungaji maarufu nchini, pamoja na waimbaji wa nyimbo za Injili waliopamba jukwaa kwa uimbaji wa kusisimua uliojaa upako.

Katika hatua ya kugusa hisia, Dk Christine alikabidhi tuzo maalum ya upendeleo kwa mama yake mzazi, Bernadetha Kanyankole, kwa mchango wake wa kipekee wa kimalezi na kiroho.

“Tuzo hii ni ya kipekee kwa mama yangu ambaye amenilea katika msingi wa kumtumikia Mungu. Bila yeye, nisingekuwa hapa leo,” amesema kwa sauti ya hisia.

Kwa mara ya kwanza kufanyika, tuzo hizo zimepokelewa kwa shangwe kubwa, zikiahidi kugeuka kuwa tukio la kila mwaka.”Ni mwanzo tu huu,” amehitimisha Dk Christine. “Tutakuwa tukitoa tuzo hizi kila mwaka — kadiri Mungu atakavyotuongoza!”

Related Articles

Back to top button