Muziki

Rose Mhando: Siwezi kuimba Injili kwa mahadhi ya Singeli

DAR ES SALAAM:MSANII nguli wa muziki wa Injili nchini, Rose Muhando maarufu kama Malkia wa Injili, amesema hawezi kuimba nyimbo za Injili kwa mahadhi ya Singeli, kwa kuwa hana amani moyoni anapojaribu kufanya hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa tamasha la Mtoko wa Pasaka, Rose alieleza kuwa uimbaji wake hutokana na sauti ya Mungu anayomwelekeza kutoka ndani ya moyo wake.

“Binafsi siwezi kuimba wimbo wa Injili kwa mahadhi ya Singeli hata siku moja. Ninachoimba mimi ni kile ambacho sauti ya Mungu inanieleza kutoka moyoni mwangu. Nikishaimba hivyo, moyo wangu huwa na amani,” alisema Rose.

Hata hivyo, alieleza kuwa haoni ubaya kwa waimbaji wengine wa Injili kutumia mtindo huo wa Singeli ikiwa wana amani mioyoni mwao na wanahisi kuwa ni njia wanayoongozwa na Mungu.

“Kama kuna waimbaji wanaoimba Injili kwa mfumo wa Singeli na wana amani mioyoni mwao, basi sawa. Kila mtu Mungu kamtoa mahali fulani, na kila mtu ana sauti ya kipekee kutoka kwa Mungu. Ila kwa upande wangu, siwezi,” alisisitiza.

Katika mahojiano hayo, Rose pia alisisitiza kuwa kila mtu anamjua Mungu anayemtumikia, na ni Mungu peke yake anayejua nafasi ya kila mmoja na dhamira ya moyo wake.

Aidha, Rose Mhando alitumia nafasi hiyo kumpongeza msanii wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’, kwa kufanya challenge ya kucheza wimbo wake, akiomba baraka za Mungu zimshukie kijana huyo katika kazi zake.

“Nimefurahi sana kumuona kijana wangu Harmonize akicheza wimbo wangu. Mungu ambariki sana katika kazi zake. Nimependa sana alivyoonyesha heshima na mapenzi kwa kazi yangu,” alisema kwa bashasha.

Tamasha la Mtoko wa Pasaka lililofanyika katika ukumbi wa The Super Dome, lilikutanisha waimbaji mbalimbali wa Injili, mashabiki, viongozi wa dini, na watu mashuhuri kutoka sekta mbalimbali akiwemo Mtumishi wa Mungu Mwampona na Irene Uwoya.

Related Articles

Back to top button