La Liga

Real Madrid yaachana na Alonso

MADRID:REAL Madrid wametangaza kuachana na kocha Xabi Alonso kwa makubaliano ya pande zote, siku moja tu baada ya kupoteza fainali ya Spanish Super Cup kwa kufungwa mabao 3-2 na wapinzani wao wakubwa Barcelona. Taarifa ya klabu imesema Alonso ataendelea kubaki kuwa sehemu ya familia ya Real Madrid, lakini safari yake kama kocha wa kikosi cha kwanza imefikia mwisho mapema kuliko wengi walivyotarajia.

Alonso anaondoka baada ya kukaa Santiago Bernabeu kwa zaidi ya miezi saba tu tangu alipoteuliwa Mei mwaka jana, baada ya kuvutia sana akiwa Bayer Leverkusen. Hata hivyo, mambo hayakwenda kama ilivyotarajiwa. Matokeo mabaya kwenye mashindano mbalimbali, pamoja na ripoti za mvutano ndani ya chumba cha kubadilishia nguo, zilianza kuigawa timu mapema.

Katika kipindi chake, Real walipata vipigo vizito dhidi ya PSG kwenye Kombe la Dunia la Klabu, Atletico Madrid LaLiga, pamoja na Liverpool na Manchester City kwenye Ligi ya Mabingwa. Licha ya kuongoza LaLiga mapema kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Barcelona, timu ilianguka kiwango na sasa ipo nafasi ya pili, pointi nne nyuma ya Barca.

Kuondoka kwake kunakuja kama ishara nyingine ya namna Real Madrid isivyopenda kusubiri pale matokeo yanaposhuka. Mradi uliokuwa unaonekana wa muda mrefu umevunjika mapema tofauti na matarajio ya mashabiki.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button