RC Makalla na mkakati wa kuifufua Pamba

HUENDA ile burudani ya mchezo wa soka kutoka kwa timu ya Pamba (wana TP lindanda) sasa inaweza ikarejea kwa kasi kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuanza kucheza Ligi Kuu.
Hii ni baada ya timu hiyo kukaa benchi kwa zaidi ya miaka 20 pasipo kushiriki kwenye michuano ya Ligi Kuu ambayo ilitamba katika miaka ya 90 ikiwa imesheheni wachezaji waliong’ara na kutamba wakichezea Yanga, Simba na timu ya Taifa.
HISTORIA YAKE
Timu hiyo ilikuwa miongoni mwa klabu maarufu za soka, iliyokuwa haikosekani katika orodha ya waliowahi kuwa miongoni mwa mabingwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ilikuwa ni ‘ghala na hazina’ ya wachezaji wengi waliowahi kuichezea timu ya taifa, waliong’ara katika miaka ya 90 ni John Makelele, Rajabu Risasi, Ibrahim Magongo, Isack Mwakatika, Hussein Masha, George Magere Masatu na Fumo Felician.
Pamba iliacha kucheza Ligi Kuu mwaka 1999 ikiwa ni chimbo la wachezaji mahiri na kimbilio la klabu kubwa nchini, ikilisakata kandanda la burudani la “kampa, kampa tena”, ambalo tokea enzi hizo limekuwa maarufu sana kwa klabu mbalimbali za soka.
LIGI KUU/NDOTO
Ndoto hizo zinakwenda kutimia, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla ambaye gazeti la HabariLEO Jumamosi inatoa kongole kwake, kuja na mkakati madhubuti wa kisayansi wa kuinusuru Pamba.
Makalla aliyasema hayo baada ya kuikabidhi timu hiyo hivi karibuni kwa uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza ili waweze kuiendesha na iweze kucheza ligi kuu.
MKAKATI vs MAKALLA
Makalla ambaye ni mwanamichezo akitokea Morogoro, kwa hakika amedhihirisha yeye ni Makalla wa Morogoro, mkoa wenye vipaji na vipawa vya soka miaka dahari, ukizalisha wanasoka nguli na mashuhuri waliopata kuiletea nchi heshima.
Mkoa wenye kila aina ya wanyama wakiwemo wachezaji wa mpira waliojulikana kwa unyama wao uwanjani wakiwemo Hussein Ngulungu, Jela Mtagwa na Gibson Sembuli kwa kutaja wachache.
Uzoefu na utashi wa Makalla katika soka na michezo mingine, unahamia rasmi Mwanza kwa kuanza kupiga jaramba ya kuonesha nia yake ya kuifufua timu ya Pamba yumkini na michezo mingine!
Katika hili, Makalla amevuna bingo sio tu kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, bali kwa taifa kwa sababu michezo ni afya, furaha na uchumi.
Makalla alisema kipaumbele chake katika mchezo wa soka ni kuiona Pamba na timu nyingine zilizo katika Mkoa wa Mwanza zinaimarika na kucheza Ligi Kuu na kwamba Mkoa wa Mwanza una miundombinu mizuri, Chuo cha Michezo Malya, vipaji lukuki na haoni sababu usiwe na timu inayocheza ligi kuu.
Anasema ameirejesha Pamba Halmashauri ya Jiji la Mwanza iweze kujiendesha kwa ufanisi, kutatua changamoto za kifedha sanjari na kuirejesha kwa wananchi kama ilivyokuwa chini ya Bodi ya Pamba Tanzania (TCB).
KWANINI JIJI LA MWANZA?
Alisema baada ya kukabidhiwa rasmi timu ya pamba, alikutana na uongozi wa Halmashauri
ya Jiji la Mwanza na kuwauzia wazo la kuimiliki na kuiendesha timu hiyo, ambalo kimsingi walilikubali kwa mikono miwili.
Alihimiza mchakato wa kuundwa kamati ya mpito kwa uongozi wa timu hiyo na Jiji la Mwanza ili kukamilisha hatua zote muhimu za usajili ikiwemo suala la usajili wa wachezaji.
Aliwataka wananchi na wadau wa soka mkoani kushikamana pamoja ili kuiwezesha Pamba kucheza Ligi Kuu ikiwemo na uboreshaji wa michezo mingine pia.
Alipowasili jijini Mwanza, alisema ndoto yake ni kuuona Mkoa wa Mwanza unapata timu zinazocheza ligi kuu. Alisema haitakuwa na maana yeye kuwa mdau wa michezo halafu asifanye jitihada za kuhakikisha wakazi wa mkoa huo wanapata timu itakayokuwa ikiwaletea burudani ya soka na mapato yatokanayo na michezo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Aaron Kagurumjuli alisema halmashauri iko tayari kusimamia Pamba vizuri kwenye soka na iweze kufanya vizuri kwenye ligi kuu.
WASEMAVYO VIONGOZI/ WADAU/WACHEZAJI WA ZAMANI
Mwenyekiti wa MZFA Mkoa wa Mwanza, Vedastus Lufano alisema wao kama viongozi
wa soka wamefarijika sana kwa hatua iliyochukuliwa na Mkuu wa Mkoa katika kuisaidia timu hiyo ya Pamba.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Pamba, Evaristi Hagilla alisema hatua iliyochukuliwa na Mkuu wa Mkoa ina manufaa makubwa kwa madai kuwa katika kuiongoza timu, kunahitajika fedha, uongozi na usimamizi mzuri.
Mdau wa soka na mpambanaji wa timu ya Pamba kwa takribani miaka minne, Ally Msoya anasema hatua iliyochukuliwa na Makalla anaiunga mkono kwa asilimia 100. Anasema hatua hiyo inakuja na mpango mahususi wa kuiendeleza Pamba ambayo kwa sasa itakuwa
ikiendeshwa kwa kufuata utaratibu wa maamuzi ya vikao.
“Huko nyuma timu ya Pamba ilikuwa ikiendeshwa kwa maamuzi ya mtu mmoja, kwa mtindo huo isingeweza kufanikiwa,” anasema Msoya na kuongeza: “Ushauri wangu kwa
Mkuu wa Mkoa na uongozi wa Jiji la Mwanza ili mkoa usiingie kwenye changamoto zilizotokea kwa KMC na Mbeya City, iundwe kamati itakayoshirikisha wadau wa mkoa wenye uchumi mkubwa ili kuisaidia Pamba maana mpira bila fedha ni vigumu kuendesha timu,” anasema.
“Lazima tuseme ukweli kwa sababu watu wengi wamelia machozi kuona timu ya Pamba haipandi Ligi Kuu,” anasema Msoya. Katibu wa wandishi wa habari za michezo Mkoa wa Mwanza, Fabian Fanuel anapongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na Makalla ya kuikabidhi timu hiyo kwa uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Katibu wa Nidhamu wa MZFA, Rashid Rato alisema kitendo kilichofanywa na Makalla cha kuikabidhi timu hiyo kwa uongozi wa jiji anakikubali kwa asilimia 100.
Mchezaji wa zamani wa timu ya Pamba, Fumo Felician (1987-1992) na baadaye timu ya Yanga na timu ya Taifa, Fumo Felician anasema yeye binafsi na wadau wa soka wamepokea kwa furaha kubwa uamuzi huo uliochukuliwa na Makalla.
“Nakumbuka Pamba wakati ilikuwa ikifanya vizuri kwenye soka na wakati tulikwenda kucheza na Coastal Union ya Tanga mwaka 1989 tulikwenda kwa ndege ya kukodi,” anasema Felician.