PSG yamtambulisha Dembele

KLABU ya Paris Saint-Germain imemsajili fowadi wa Ufaransa, Ousmane Dembele kutoka Barcelona kwa pauni milioni 43.5 sawa na shilingi bilioni 133.67.
Amesaini mkataba wa miaka mitano kuwatumikia mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligue 1.
Dembele mwenye umri wa miaka 26 alijiunga na Barcelona mwaka 2017 kutoka Borussia Dortmund kwa ada ya pauni milioni 135 na amefunga mabao 40 katika michezo 185 akishinda mataji matatu ya La Liga na mawili ya Copa del Rey.
“Nina furaha sana kujiunga na Paris St-Germain na nasubiri kwa hamu kucheza katika rangi yangu mpya. Natumaini naweza kuendelea kukua hapa na kuwafanya mashabiki wote wa klabu kujivunia,” amesema Dembele.
Mapema wiki hii Kocha wa Barca, Xavier Hernández alithibitisha kwamba Dembele anataka kuondoka klabu hiyo.