P.Diddy ashinda tena kesi nyingine

NEW YORK: MWANAMUZIKI na mfanyabiashara mashuhuri Sean ‘Diddy’ Combs amepata ushindi wa kisheria katika kesi yake inayoendelea nchini Marekani, baada ya mahakama kuridhia ombi lake la rufaa ya haraka (expedited appeal) hatua ambayo inaweza kuharakisha usikilizwaji wa hoja zake kufikia Aprili 2026.
Uamuzi huo unampa Combs, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miezi 50 kwa makosa ya usafirishaji wa watu kwa ajili ya ukahaba, nafasi ya kupinga baadhi ya vipengele vya hukumu yake kabla hajamaliza sehemu kubwa ya kifungo hicho.
Timu yake ya wanasheria ilieleza kuwa mchakato wa kawaida wa rufaa nchini Marekani ambao unaweza kuchukua miezi 12 hadi 18 ungeweza kufanya matokeo yoyote yawe hayana maana endapo angekuwa amekwishakaribia kumaliza adhabu yake.
Kwa mujibu wa Fox News, mahakama ilisisitiza kuwa uamuzi huo haukuashiria mashaka juu ya ushahidi au hukumu bali ulikusudia kuhakikisha kuwa mchakato wa rufaa unabaki na umuhimu wa kisheria.
Mwendesha mashtaka wa zamani wa serikali ya shirikisho, Neama Rahmani, ambaye sasa anaongoza kampuni ya West Coast Trial Lawyers, alisema mahakama imetambua umuhimu wa kuhakikisha kesi inasikilizwa mapema, kwani uamuzi wowote wa baadaye ungepoteza uzito kama Diddy angekuwa tayari ametumikia sehemu kubwa ya kifungo.
Rahmani aliongeza kuwa hatua hii inaweza pia kumpa Diddy fursa ya kuomba kuhamishiwa katika nyumba ya uangalizi (halfway house) au kifungo cha nyumbani mapema kuliko ilivyotarajiwa.
Wanasheria wa Diddy pia wanaripotiwa kuchunguza uwezekano wa kupunguza adhabu kupitia njia nyingine, ikiwemo msamaha wa rais kutoka kwa Donald Trump.
Wakili wa utetezi wa jinai, Nicole Blank Becker, alisema msamaha wa Trump si jambo lisilowezekana, ikizingatiwa historia yake ya kuwapa msamaha watu mashuhuri waliowahi kukumbwa na kesi nzito.
Hata hivyo, aliongeza kuwa mchakato wa msamaha huo si rahisi, kwani Diddy atalazimika kuonesha majuto ya dhati na kuepuka kuonekana kama anapingana na mfumo wa sheria.
Kwa mujibu wa Becker, maombi mengi ya msamaha wa urais hushughulikiwa kwa siri, kupitia watu wenye ushawishi wa kisiasa.
Rais Donald Trump (79) amekiri kuwa Diddy aliwasilisha ombi la msamaha, na akasema yuko tayari kulichunguza endapo ataamini kesi hiyo ilishughulikiwa kwa haki.
Vyanzo vya habari kama TMZ vinaripoti kuwa Combs ana imani kubwa kuwa Trump atampa msamaha ifikapo mwaka 2026.
Kesi yake ya wiki nane mapema mwaka huu ilisababisha kufutiwa kwa mashtaka ya ulanguzi wa ngono na uhalifu wa magenge, lakini alihukumiwa kwa makosa yanayohusiana na ukahaba.
Wataalamu wa sheria wamesema rufaa ya haraka ni “mwanga wa matumaini” kwa Diddy, japo sio dhamana ya kupunguziwa adhabu. Inampa nafasi ya kuwasilisha hoja zake kabla muda wake wa kifungo haujakaribia kuisha.
Mwanzilishi wa Bad Boy Records kwa sasa anatumikia kifungo chake katika gereza la Federal Correctional Institution, Fort Dix, na ameamriwa kulipa faini ya takriban $500,000 (Sh65 milioni).
Baada ya kuachiliwa, Diddy atakuwa chini ya usimamizi wa majaribio kwa miaka mitano, huku tarehe yake rasmi ya kuachiliwa ikiwa 8 Mei 2028




