
Nyimbo za wanamuziki wa Kitanzania zitapigwa kwa asilimia 100 kwenye viwanja vya ndege nchini kufuatia makubaliano ya Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege.
Katika kikao kilichofanyika Jijini Dar es Salaam, Mwana FA, ametoa rai kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Musa Mbura, kuhakikisha nyimbo za wanamuziki wa Kitanzania zinapigwa kwa asilimia 100 kwenye viwanja vya ndege.
Hatua hii inalenga kuendelea kutangaza utamaduni wa muziki wa Kitanzania kwa wageni wanaoingia na kutoka nchini.
Kikao hicho cha kazi kilishirikisha viongozi wa ngazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa, Dkt. Emmanuel Ishengoma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Dkt. Kedmon Mapana, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dkt. Kiago Kilonzo, na Kaimu Mtendaji Mkuu wa COSOTA, Baraka Katemba.