Africa

“Njooni kwa wingi tumkaribishe Pantev” – Ahmed Ally

DAR ES SALAAM: MSEMAJI wa Simba SC, Ahmed Ally, ametoa wito kwa mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini, utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, akisisitiza kuwa mechi hiyo ni ya kihistoria kwa timu na kwa kocha mpya, Dimitar Pantev.

Ahmed alisema ni muda wa mashabiki kuungana tena na timu yao, hasa baada ya kutoshiriki kikamilifu katika mechi za awali za michuano hiyo kutokana na adhabu ya kucheza bila mashabiki.

“Ni muhimu sana mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huu. Msimu huu mashabiki hawajapata nafasi ya kuwa bega kwa bega na timu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Tunahitaji ushindi wa kishindo mbele ya umati mkubwa wa mashabiki,” alisema Ahmed.

Amefafanua kuwa mchezo huo pia utakuwa fursa maalum ya kumkaribisha rasmi kocha mpya wa timu hiyo, Dimitar Pantev, ambaye hadi sasa hajawahi kuonekana mbele ya mashabiki wa Simba kutokana na kufungiwa katika mchezo wa awali dhidi ya Gaborone United.

Huu utakuwa mchezo wa kwanza wa Pantev kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Ni fursa ya mashabiki wetu kumkaribisha Tanzania, Dar es Salaam, na ndani ya familia ya Simba SC. Tunataka iwe Simba Day ya Dimitar Pantev,” alisema Ahmed.

Ameongeza kuwa kocha huyo hajawahi kushuhudia umati mkubwa wa mashabiki uwanjani, kwani amewahi kufundisha katika ligi za Cameroon na Botswana ambazo hazina uungaji mkono mkubwa wa mashabiki kama Tanzania.

“Sasa amekuja kwenye ukanda wa soka la ushindani na timu yenye mashabiki wengi kama Simba. Ni jukumu letu kumwonesha kuwa yuko mahali salama na sahihi — na hilo linawezekana tu tukijitokeza kwa wingi na kulipa viingilio,” aliongeza kwa msisitizo.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa ugenini Eswatini wekundu hao walishinda mabao 3-0 na kutanguliza mguu mmoja hatua ya makundi.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button