Nicolas Jackson ni ‘The Blues’

KLABU ya Chelsea ‘The Blues’ imetangaza kumsajili mshambuliaji Nicolas Jackson kutoka Villarreal ya Hispania kwa mkataba wa muda mrefu.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Senegal amesaini mkataba wa miaka nane Stamford Bridge na ni usajili wa pili wa timu hiyo chini ya kocha Mauricio Pochettino baada ya Christopher Nkunku kutoka RB Leipzig.
Tovuti ya michezo ya 90min imesema Chelsea imekubali kuilipa Villarreal zaidi ya Euro milioni 35 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 89 za kipengele cha kuachiwa Jackson lakini zitalipwa kwa mafungu.
“Nahisi nitafanya mambo makubwa hapa,” amesema Jackson kupitia taarifa yake kwa njia ya video.
Jackson mwenye umri wa miaka 21 alikaribia kuhamia England mwezi Januari wakati timu ya Bournemouth ilipokubali kumsajili lakini uhamisho ulikwama baada ya kushindwa vipimo vya afya.
kufuatia kukwama kwa uhamisho huo Jackson alichukua jukumu muhimu Villarreal huku magoli tisa kati ya 12 katika La Liga akifunga katika michezo nane ya mwisho msimu wa 2022/23.