Nico na neno zito kwa United

BILBAO, Winga wa Athletic Bilbao Nico Williams amesema timu yake itajitoa “mwili na roho” ili kuifunga Manchester United watakapokutana kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Europa League siku Alhamisi na wao kutinga fainali ya Europa League.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Spain amesema yeye na wachezaji wenzake wana ndoto ya kucheza Fainali ya michuano hiyo ambayo itaandaliwa kwenye uwanja wao wa San Mames baadae mwezi Mei. Winga huyo alienda mbali na kusema kuwa timu hiyo imekuwa ikifuata ushauri wa kaka yake na mchezaji mwenzake klabuni hapo Inaki Williams wakati wote mbio zao za Ligi ya Europa League msimu huu kutokana na uzoefu wake.
“Tangu mwanzo tumekuwa watulivu, kaka yangu alituambia mwaka jana ni lazima tuwe watulivu. Ninaelewa furaha ya mashabiki, lakini tunahitaji kuelekeza nguvu zetu kwa asilimia 100 kwenye mchezo huu ni kazi yetu. Tutatoa miili na roho zetu ili tufike fainali kwenye uwanja wetu wa San Mames” – Nico Williams alisema.
Athletic watawakaribisha vijana wa Ruben Amorim Manchester United katika uwanja wa San Mames kesho Alhamisi katika mechi ya nusu fainali ya kwanza, kabla ya kurudiana nao Old Trafford wiki ijayo.