Namungo kinara kutema wachezaji

LINDI: KLABU ya Namungo ni kama wamedhamiria ubaya hivi katika dirisha dogo la usajili, wauaji hao wa kusini wamepiga panga la maana ndani ya timu hiyo huku wakitarajiwa kuongeza majembe mengine.
Ifahamike kwamba vijana hao wananolewa na kocha mwenye uzoefu katika soka la Bongo, Juma Mgunda hivyo wanatazamwa kama timu itakayoreja kwa kishindo katika duru ya pili ya ligi hiyo namba sita kwa ubora Afrika.
BEKI wa zamani wa Yanga Djuma Shabani ni miongoni mwa wachezaji wanne waliotemwa na Namungo.Shabani alijiunga na klabu hiyo kama mchezaji huru Julai 2024 na hata hivyo, jina lake halikuvuma sana kama alivyokuwa kunako klabu yake ya zamani ya Yanga na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Namungo kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii ilitangaza kuachana na mchezaji huyo.
“Asante Djuma Shabani kwa kipindi chote ulichokuwa nasi wauaji wa Kusini. Tunakutakia kila la kheri kwenye majukumu yako mapya popote utakapokuwa,”ilisema taarifa ya klabu hiyo.
Wengine waliotemwa ni mkongwe Frank Domayo aliyewahi kuzitumikia Yanga na Azam kwa vipindi tofauti. Ritch Nkoli na Amza Ngamchiya pia, wamo.