Nabi: Tunajua bado hatujafuzu

KOCHA Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amewataka wachezaji wa timu hiyo kutobweteka na matokeo ya mchezo wa kwanza Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rivers United badala yake washinde tena mchezo wa marudiano Aprili 30.
Akizungumza Dar es Salaam leo kuelekea mchezo huo wa marudiano kwenye uwanja wa Bnejamin Mkapa, Dar es Salaam Nabi amesema wachezaji wote wako vizuri, wanajituma mazoezini na timu inajua kuwa inahitaji matokeo mazuri katika mchezo huo ili kwenda hatua inayofuata.
“Nimekaa na wachezaji wangu na tumekubaliana kuwa kazi nzuri tuliyofanya Nigeria itakuwa hauna maana kama hatutashinda mchezo wa kesho,” amesema Nabi.
Yanga ilishinda mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Aprili 23 kwenye uwanja wa Godswill Akpabio uliopo mji wa Uyo, Jimbo la Akwa Ibom Kusini mwa Nigeria.