Mwigulu: Samia ana mchango kwenye michezo

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango anaotoa katika kuinua michezo nchini.
Dkt Mwigulu ametoa pongezi hizo leo wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/24.

“Vilevile, naomba kutambua mchango na hamasa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kutoa motisha kwa timu zetu za michezo pale zinapofanya vizuri kimataifa, “amesema Dkt. Mwigulu.
Dkt. Mwigulu pia amezipongeza klabu za Yanga na Simba kwa kuliwakilisha taifa vema katika michuano ya kimataifa.
“Kwa hakika, timu hizi zimeliheshimisha Taifa letu katika nyanja za kimataifa. Mafanikio hayo ya timu za Yanga na Simba yamepandisha hadhi ya Taifa letu katika viwango vya mpira wa miguu vinavyosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika – CAF,”ameongeza Waziri huyo wa Fedha na Mipango.
Simba iliwakilisha taifa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuishia hatua ya robo fainali wakati Yanga ilikuwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilifika hatua ya fainali.