Tetesi

Mwelekeo wa Mbappe ni upi?

SWALI kubwa ambalo mpaka sasa halina majibu huko barani Ulaya ni kwamba wapi ataelekea mshambuliaji wa Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe,  baada ya habari kuwa klabu hiyo inapanga kumuuza Mfaransa huyo msimu huu wa majira ya joto.

Kwa mujibu wa mtandao wa Shirika la Habari Uingereza-BBC hatua hiyo ni baada ya PSG kuhofia huenda ikampoteza bure mchezaji huyo kwa kuwa umebaki mwaka mmoja katika mkataba wake huku akigoma kuongeza mkataba mwingine.

Awali kulikuwa na habari kuwa tarehe Julai 31, 2023 ni tarehe ya mwisho kwa Mbappe mwenye umri wa miaka 24 kuwaambia PSG kama atabaki klabu hiyo hadi 2025. Baada ya mazungumzo miezi kadhaa, Mbappe alitoa barua kuwa hatofanya hivyo.

Hata hivyo, wakati mabingwa hao wa Ufaransa wakijaribu kurekebisha sera yao ya ujenzi wa timu baada ya miaka mingi ya kununua wachezaji nyota bila mkakati madhubuti, PSG imeazimia kutomwachia Mbappe bure, huku klabu hiyo ikikerwa na barua hiyo kuvujishwa kwenye vyombo vya habari kabla.

Real Madrid inamtamani kwa muda mrefu Mfaransa huyo na mwaka jana alikataa kuhamia Bernabeu hivyo kusalia PSG.

Kuondoka kwa Karim Benzema katika klabu ya Real Madrid kwenda Saudi Arabia kunamaanisha kuwa Real inahitaji mshambuliaji, ingawa ilifikiriwa kuwa Harry Kane wa Tottenham alikuwa kipaumbembele miongoni mwa orodha.

Mbappe, ambaye alijiunga na PSG mwaka 2017 kwa mkopo akitokea Monaco kabla ya uhamisho wa Euro milioni 180 sawa na shilingi bilioni 452, amefunga mabao 212 katika michezo 260.

Ana mabao 38 katika mechi 68 alizoichezea Ufaransa, ikiwa ni pamoja na hat-trick katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia Qatar 2022, Ufaransa iliposhindwa na Argentina kwa mikwaju ya penalti.

Mbappe amekuwa mfungaji bora wa Ligue 1 misimu mitano iliyopita na ameshinda mataji matano ya ligi katika misimu yake sita akiwa PSG.

Related Articles

Back to top button