Mwana FA aipa sapoti Simba, Afrika Kusini

AFRIKA KUSINI: NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, Mwana FA, amewasili nchini Afrika Kusini kuungana na wawakilishi wa Tanzania, klabu ya Simba SC, katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch FC.
Mwana FA ametua leo mchana jijini Johannesburg, Afrika Kusini, kabla ya kuelekea moja kwa moja jijini Durban ambako mchezo huo wa marudiano utafanyika Jumapili, Aprili 27 kwenye Uwanja wa Moses Mabhida.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, Simba ilijipatia ushindi wa bao 1-0, na sasa inahitaji sare au ushindi ili kutinga hatua ya fainali ya mashindano hayo ya kimataifa.
Katika safari hiyo ya kuunga mkono timu ya Simba, Mwana FA ameambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Hamis Taletale, Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF Athumani Nyamlani pamoja na baadhi ya mashabiki wa Simba waliowasili kwa lengo la kushangilia na kuipa nguvu timu yao.
Simba inawakilisha matumaini ya Watanzania wote katika mashindano haya na Serikali imeonyesha mshikamano kwa kuungana na mashabiki katika kuiunga mkono klabu hiyo kuelekea mafanikio ya kihistoria.