Mwakinyo: Nipo tayari kupambana na bondia yeyote

DAR ES SALAAM: BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo, amesema yupo tayari kupanda ulingoni kupambana na bondia yeyote endapo maslahi yatakuwa ya kuridhisha.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuelekea pambano lake lijalo la Boxing on boxing Day, linalotarajiwa kufanyika Desemba 26 mwaka huu, Mwakinyo amesema anaamini uwezo wake mkubwa ulingoni unamwezesha kukabiliana na mpinzani yeyote.
“Nipo tayari kupigana na bondia yoyote, ilimradi maslahi yawiane na kile ninachostahili. Mimi ni bondia mwenye uwezo mkubwa na ninaendelea kujifua kuhakikisha nafanya vizuri,” amesema Mwakinyo.
Kwa sasa, Mwakinyo yuko kwenye kambi ya mazoezi akijiandaa kwa pambano hilo, huku mpinzani wake akitarajiwa kutangazwa hivi karibuni.
Kwa upande wake, Mratibu wa pambano hilo kutoka kampuni ya Peak Time Sports Agency, Bakari Khatibu, amesema sababu ya kupeleka pambano hilo Mwanza lengo kuu ni kuinua vipaji vya mabondia kutoka Kanda ya Ziwa sambamba na kuendeleza mchezo wa ngumi nchini.
“Tunataka kuwapa nafasi mabondia wa kanda hii kuonesha uwezo wao. Pia ni fursa nzuri ya kuitangaza ngumi na kuleta hamasa kwa mashabiki,” amesema.
Ameongeza kuwa jina la mpinzani wa Mwakinyo litatangazwa muda si mrefu ili mashabiki na wadau wa mchezo huo waweze kufuatilia maandalizi ya pambano hilo kikamilifu.