Mwakinyo autamani mkanda wa WBO

BONDIA wa Tanzania, Hassan Mwakinyo amesema kwa morali aliyonayo katika mazoezi
ya pambano lake la kimataifa anatamani kutwaa mkanda wa dunia wa WBO.
Mwakinyo anatarajiwa kupanda ulingoni Septemba 3 mwaka huu kupigana na Liam Smith wa Uingereza mjini Liverpool.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Mwakinyo amesema namna anavyopata morali akiufikiria mkanda huo anaokwenda kuupigania siku hiyo.
“Mara kadhaa najiwa na morali sana kila nikitafakari juu ya usiku ambao nitatangazwa kuwa bingwa wa WBO rasmi kutoka Makorora Tanga Tanzania,” amesema.
Nyota huyo aliyehamishia makazi yake Marekani amekuwa akijifua katika mazoezi ya nguvu kuhakikisha anatimiza ndoto yake.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, amekuwa akiweka picha zinazomwonesha namna anavyofanya mazoezi ya nguvu kiasi cha kupata vidonda kwenye vidole ikionesha wazi anajipanga vyema kwenda kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Mwakinyo mwenye nyota tatu na nusu anacheza na mwenzake mwenye nyota nne ambaye ni mzoefu akiwa amecheza mapambano mengi zaidi ya 35 na kati ya hayo ameshinda 31, amepoteza matatu na kupata sare moja huku Mtanzania huyo akicheza 22 na kati ya hayo, ameshinda 20 na kupoteza mawili.
Iwapo atashinda atazidi kupanda viwango vya kimataifa na itakuwa ni mara ya pili anampiga bondia kutoka Uingereza baada ya mwaka 2018 kumpiga Sam Eggington kwenye pambano lililopigwa katika mji wa Birmingham.