Muogeleaji Michael aula Ufaransa

MUOGELEAJI wa klabu ya Taliss Michael Joseph amepata ufadhili wa mwaka mmoja wa kwenda kwenye mafunzo ya kuogelea nchini Ufaransa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA) mchezaji huyo atashiriki mafunzo kwenye kituo cha michezo cha Antibes.
Mchezaji huyo anatarajiwa kuondoka leo kwa ajili ya kuanza safari hiyo ya mafunzo ya mwaka mmoja kama ilivyoelezwa kwenye barua.
TSA imemtakia kila la heri mchezaji huyo atimize malengo yake ya kujifunza zaidi mchezo huo na kufanya vizuri hapo baadaye katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Taarifa hiyo iliwekwa katika akaunti ya mtandao wa kijamii ya Baba wa mchezaji huyo Jose Mara ambaye amesema siku zote bidii huwa ina malipo akimpongeza kijana wake kwa hatua hiyo.
“Asante sana kwa jitihada zako, Ufaransa naomba mumpokee kijana anakuja kwa ajili ya kuongeza ujuzi zaidi, imesema taarifa ya mzazi wake.