Muigizaji wa Kenya Bilal Wanjau afariki dunia

NAIROBI: SEKTA ya filamu na maigizo nchini Kenya imetangaza kusikitishwa na kifo cha muigizaji mahiri, Bilal Wanjau.
Muigizaji Sandra Dacha, amesema Wanjau alifariki dunia leo, Desemba 4, 2025, wakati akipatiwa matibabu katika hospitali moja huko Nairobi kutokana na matatizo ya kisukari.
“Ni kwa huzuni kubwa kwamba napenda kuwatangazia kumpoteza ghafla mwenzetu Bilal Wanjau asubuhi hii kutokana na matatizo ya kisukari,” Sandra alieleza.
Sandra aliongeza kwa masikitiko makubwa kuhusu kifo chake, akisema kuwa tasnia imepoteza mmoja wa waigizaji bora zaidi katika ulingo wa filamu nchini Kenya.
“Bilal alikuwa muigizaji mwenye kipaji kikubwa! Tumepoteza mmoja wa waigizaji bora kabisa katika tasnia,” alieleza.
Alifichua pia kuwa maandalizi ya maziko yamekamilika, na Wanjau atazikwa kwesho Ijumaa, Desemba 5, 2025, nyumbani kwao kijijini Machakos.
“Maziko yatafanyika Ijumaa kesho, nyumbani kwake kijijini Machakos. Tafadhali kuwaombea familia yake,” alieleza.
Bilal Wanjau alifurahia safari ndefu ya sanaa, akitokea kwenye maonesho maarufu ya televisheni na filamu ya Kenya. Alijulikana sana kwa mchango wake katika filamu kama ‘Tahidi High’, ambako uchezaji wake uliacha kumbukumbu ya kudumu kwa watazamaji.
Kwa miaka mingi, alicheza katika tamthilia na filamu mbalimbali za nyumbani, ikiwa ni pamoja na ‘Bazenga’, ‘The Runaway’, na ‘Wimped’. Pia alicheza katika ‘Lies That Bind’ na tamthilia ya ‘Jela 5 Star’.




