Nyumbani

Msigwa akabidhi milioni 15 Simba

DAR ES SALAAM: KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amekabidhi kiasi cha sh milini 15 kwa timu ya Simba ikiwa ni zawadi ya goli la Mama inayotolewa na Rais wa Samia Suluhu Hassan.

Simba wamekabidhiwa fedha hizo Dar es Salaam leo kufuatia ushindi waliopata katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika wa mabao 3-0 dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Leo tumekuja hapa Bunju, viwanja vya mazoezi ya Simba, kukabidhi fedha za Goli la Mama. Rais Samia amesisitiza kuwa si fedha pekee, bali ni pongezi na motisha kwa wachezaji kuhakikisha wanawakilisha vyema Tanzania kimataifa,”alisema.

Alisema Rais Samia ana imani kubwa na Simba katika mashindano ya mwaka huu kuwa watafika fainali.

Msigwa alisema licha ya kuwa Rais Samia yupo kwenye kampeni kuelekea uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, kila mara timu inapocheza, yeye lazima atazame.

Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi Simba Crescentius Magori alimshukuru Rais Samia kwa motisha hiyo na kuahidi kuwa watapambana zaidi katika mechi zinazofuata.

“Tumepewa motisha kubwa na Rais, tunawaahidi Watanzania na Mheshimiwa Rais kuwa tutazidi kushinda, na Jumapili waandae fedha nyingi, kwani tutaonesha kiwango cha juu kufika fainali,” alisema Magori.

Mchezaji Shomari Kapombe aliongeza kuwa motisha waliyopewa inawapa nguvu ya ziada kuwakilisha nchi vizuri.

“Tumeyapokea maelekezo ya Rais kwa moyo wote. Tumejiandaa vizuri na tunaahidi kufanikisha ushindi, na pia kumtakia kila la heri katika uchaguzi Mkuu,” alisema Kapombe.

Related Articles

Back to top button