Kwingineko

Mshahara wamkimbiza Mosimane Iran

TEHRAN: KOCHA raia wa South Africa Pitso Mosimane ameachana rasmi na klabu ya Esteghal FC ya nchini Iran kisa ishu za mishahara ambazo kwa mujibu wa menejimenti yake zimeathiri maisha yake binafsi na familia akifikia uamuzi huo mara moja baada ya juhudi za mazungumzo na klabu hiyo kugonga mwamba.

Menejimenti inayomsimamia Mosimane ya MT sports imesema iliwasiliana na uongozi wa Esteghal FC na kufanya majadiliano kupitia CEO wa zamani wa timu hiyo tangu mwaka jana lakini klabu hiyo ilishindwa kulipa madeni hayo.

“Kwa kuzingatia miongozo ya FIFA Mosimane na benchi lake la ufundi waliipa klabu kupitia kwa CEO mpya na bodi yake siku 15 kushughulikia suala hili. Hata hivyo Esteghal hawakuweza kulipa katika kipindi hiki na Mosimane na benchi lake wamesalia bila malipo kwa miezi miwili” – imesema sehemu ya taarifa ya MT Sports.

Mosimane anaiacha Esteghal FC nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi kuu ya Iran (Persian Gulf Pro League) yenye timu 16 wakipoteza mechi 3 kati ya 10 za mwisho na kuisaidia timu hiyo kusonga mbele kwenye kombe la FA la Iran.

Mosimane alijizolea umaarufu mkubwa katika soka la Afrika baada ya kufanya maajabu akiwa na klabu ya nyumbani kwao Mamelodi Sundowns na mabingwa wa soka la Afrika Al Ahly SC.

Related Articles

Back to top button