Muziki

Msanii Irene Robert, afariki dunia

DAR ES SALAAM:TASNIA ya muziki wa Injili nchini Tanzania imepata pigo kufuatia kifo cha muimbaji maarufu Irene Robert, aliyeripotiwa kufariki dunia leo Ijumaa baada ya kuugua ghafla.

Taarifa za msiba huo zimethibitishwa na msanii mwezake, Walter Chilambo kupitia ukurasa wake wa Instagram, ambapo ameeleza masikitiko yake na kuomboleza msanii huyo aliyegusa maisha ya wengi kupitia huduma yake ya muziki.

Marehemu Irene Robert alijizolea umaarufu kupitia nyimbo kadhaa za Injili zilizopendwa na wengi, zikiwemo Sitalia (aliyoimba kwa kushirikiana na Christina Shusho),

Neno Moja, pamoja na Soja. Kupitia kazi zake, alihamasisha na kuimarisha imani za wasikilizaji wengi ndani na nje ya Tanzania.

Mbali na mafanikio yake ya muziki, Irene Robert pia aliwahi kushinda tuzo ya AFRIMMA Awards katika kipengele cha Best Female Artiste in African Inspiration Music, jambo lililodhihirisha mchango wake mkubwa katika muziki wa Injili barani Afrika.

Kifo chake ni pengo kubwa kwa familia, marafiki, na mashabiki wa muziki wa Injili.

Taratibu za mazishi zinatarajiwa kutangazwa baadaye.

Related Articles

Back to top button