Mpanzu atikisa soko la usajili

DAR ES SALAAM: UONGOZI wa Klabu ya Simba umeweka wazi kuwa kuvunja mkataba wa kiungo wao hatari Elie Mpanzu kunahitaji zaidi ya milioni 350, huku wakisisitiza kuwa mchezaji huyo atasalia klabuni kwa msimu ujao.
Taarifa hizo zimeibuka kufuatia uvumi kuwa klabu ya RS Berkane ya Morocco imeonesha nia ya kumsajili Mpanzu, ambaye amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa kikosi cha Simba katika msimu uliomalizika.
Hata hivyo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amekanusha vikali taarifa hizo na kueleza kuwa hakuna ofa rasmi iliyowasilishwa kwa ajili ya kumnunua Mpanzu kutoka kwa timu yoyote.
“Taarifa hii ni mwendelezo wa jitihada za kuzua taharuki ndani ya klabu yetu. Hakuna ofa yoyote rasmi ya Mpanzu iliyowasilishwa kwenye uongozi wetu, wala mchezaji mwenyewe hajatoa ombi la kuvunja mkataba wake,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa gharama ya kumtoa Mpanzu ni kubwa zaidi ya kiwango kinachozungumzwa mitandaoni, hivyo ni vigumu kwa klabu yoyote kuweza kumchukua kwa sasa bila kufuata taratibu rasmi.
Ahmed amefafanua kuwa katika mikakati ya Simba ya msimu ujao, wana lengo la kuimarisha kikosi kwa kuhakikisha wachezaji wao nyota wanabaki na kuongeza wengine wenye ubora zaidi kuipa timu nguvu mpya.
Kwa kauli hiyo, mashabiki wa Simba wanaweza kupata ahueni wakijua kuwa Mpanzu, mmoja wa wachezaji waliowapa matumaini msimu uliopita, bado ni mali ya Wekundu wa Msimbazi kwa msimu ujao.