Africa

Morrison, Aucho waongeza ari Yanga

KOCHA Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze ameelezea kufurahishwa kwake na kurejea kikosini wachezaji Bernanrd Morrison na Khalid Aucho baada ya kupona majeraha kuelekea mchezo wa raundi ya pili kufuzu makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

Yanga itakuwa ardhi ya nyumbani uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Oktoba 08 kucheza na miamba hiyo ya Sudan kabla ya kurudiana wiki moja baadaye na kocha huyo anaamini kazi itamalizika nyumbani.

Akizungumza na Spotileo Kaze amesema mchezo huo ni mgumu kwa timu zote mbili na kusudio la Yanga ni kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo hivyo kurudi uwanjani kwa wachezaji hao kutaongeza nguvu.

“Kocha yoyote anapenda kuwa na wachezaji wake tegemezi kwenye mchezo. Aucho na Morrison ni wachezaji ambao licha ya kuwa na uwezo mkubwa lakini wana uzoefu na mashindano haya kurejea kwao kumetuongezea ari ya kupata ushindi,” amesema Kaze.

Amesema maandalizi kwa ujumla yanakwenda vizuri na baada ya mchezo wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting, Yanga haitakuwa na muda wa kupoteza zaidi ya kuufikiria mchezo dhidi ya Al Hilal.

 

Related Articles

Back to top button