
MARRAKECH, Morocco
TIMU ya Taifa ya Morocco imetangazwa rasmi mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kubatilisha matokeo ya fainali iliyokuwa imeipa ushindi Senegal.
Awali, Senegal ilishinda fainali hiyo kwa bao 1-0 dhidi ya Morocco katika mchezo uliochezwa Januari 18, 2026, lakini ushindi huo sasa umefutwa kufuatia uamuzi wa kamati ya rufaa ya CAF.
Kwa mujibu wa CAF, Senegal imehesabika kuwa imepoteza mchezo huo kwa kufungwa mabao 3-0 kutokana na kuvunja kanuni za mashindano baada ya wachezaji wake kutoka nje ya uwanja bila ruhusa ya mwamuzi wakati wa mchezo huo.
Tukio hilo lilitokea dakika za nyongeza huku mchezo ukiwa 0-0, baada ya mwamuzi kuipa Morocco penalti iliyozua utata mkubwa. Wachezaji wa Senegal waligoma kuendelea na mchezo huo wakiongozwa na benchi la ufundi, hali iliyosababisha mchezo kusimama kwa takribani dakika 17 kabla ya kurejea tena uwanjani.
Baada ya kurejea, penalti ya Brahim Diaz iliokolewa na kipa wa Senegal, lakini Senegal walifanikiwa kupata bao la ushindi kupitia Pape Gueye katika muda wa ziada.
Hata hivyo, CAF imeeleza kuwa kitendo cha Senegal kutoka uwanjani kilikiuka kifungu cha 82 cha kanuni za mashindano, kinachosema timu inayokataa kuendelea na mchezo au kuondoka uwanjani bila idhini ya mwamuzi itahesabika kuwa imepoteza na kuondolewa kwenye mashindano.
Kifungu cha 84 kinaeleza kuwa timu hiyo itapoteza kwa mabao 3-0.
Shirikisho la Soka la Senegal limepinga uamuzi huo na kutangaza kupeleka rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), likidai kuwa uamuzi huo ni wa “kibaguzi, wa ajabu na usiokubalika” na unachafua taswira ya soka la Afrika.
Kwa upande wao, Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) limesema rufaa yao haikulenga kupinga ushindani wa uwanjani bali kuhakikisha sheria na kanuni za mashindano zinafuatwa ipasavyo.




