Kwingineko

Mo Dewji amshukuru Rais Samia kwa kuinga mkono Simba

DAR ES SALAAM: RAIS wa heshima wa Klabu ya Simba na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji (Mo Dewji), amemshukuru kwa dhati Rais, Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa msaada wa malazi na usafiri kwa kikosi cha Simba kilichosafiri kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch FC.

Kikosi cha Simba kimeondoka leo kuelekea Durban, Afrika Kusini, ambako kitamenyana na Stellenbosch katika Uwanja wa Moses Mabhida siku ya Jumapili, Aprili 29, kwa lengo la kutafuta ushindi utakaoipeleka timu hiyo kwenye hatua ya fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Kupitia taarifa rasmi, Mo Dewji amesema klabu ya Simba imepokea kwa shukrani kubwa msaada huo kutoka kwa Rais Samia, ambao umewezesha maandalizi bora ya safari na malazi ya timu. Alisisitiza kuwa mchango huo umeonesha namna ambavyo Serikali inajali na kuunga mkono maendeleo ya michezo nchini, hususan soka.

“Klabu ya Simba inatambua na kuthamini kwa dhati juhudi za Rais Samia katika kukuza sekta ya michezo hapa nchini. Tumetiwa moyo sana na motisha ya ‘Goli la Mama’, ambayo imekuwa chanzo kikubwa cha hamasa kwa wachezaji wetu na mashabiki,” amesema Mo Dewji.

Aidha, Dewji ameeleza imani yake kuwa benchi la ufundi na wachezaji wamejiandaa kikamilifu kwa ajili ya mchezo huo muhimu, na wataenda kupambana kuhakikisha wanapata ushindi ili kutimiza lengo la kufuzu fainali.

Vilevile, Mo Dewji alitoa shukrani kwa Wizara ya Fedha na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa kuratibu safari hiyo kwa ukaribu, pamoja na taasisi nyingine zilizoshiriki katika mchakato huo, zikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), na Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Related Articles

Back to top button