Kwingineko

MLS kuiga kalenda ya Ligi Ulaya

FLORIDA: LIGI kuu ya Marekani Major League Soccer (MLS) imepanga kufanya mageuzi makubwa kwenye kalenda yake ya mashindano kuanzia mwaka 2027, ambapo ligi hiyo itahamia ratiba ya majira ya kiangazi hadi masika mfumo unaotumika na ligi kubwa za Ulaya na hatua za mtoano (playoffs) zitafanyika mwezi Mei.

Mabadiliko hayo yataanza na msimu wa mpito kuanzia Februari hadi Mei 2027, ambao utakuwa na michezo 14 ya msimu wa kawaida, mtoano na fainali ya MLS Cup.

Msimu wa kwanza kamili chini ya mfumo mpya utaanza kati ya Julai 2027 na kuendelea hadi mwishoni mwa Mei 2028. Kutakuwa na mapumziko ya msimu wa baridi kuanzia katikati ya Desemba hadi mapema Februari, na hakuna mechi za ligi mwezi Januari.

Kamishna wa MLS Don Garber amesema uamuzi huo ni miongoni mwa maamuzi muhimu zaidi katika historia ya ligi hiyo, akibainisha kuwa ulinganifu na ratiba za kimataifa utaongeza ushindani wa klabu, kuboresha shughuli za usajili na kuhakikisha playoffs zinapata utazamajii mkubwa bila muingiliano.

Mabadiliko ya kalenda na muundo mpya wa msimu yameidhinishwa katika kikao cha Bodi ya Magavana cha MLS kilichofanyika Palm Beach, Florida, huku bodi ya ligi ikisema inaendelea kufanya kazi na Chama cha Wachezaji wa MLS (MLSPA) kutengeneza mpango wa mpito, pamoja na kuangalia marekebisho yanayowezekana ya mfumo wa playoffs.

Chini ya ratiba mpya, MLS inatarajia mechi nyingi kubaki ndani ya dirisha la hali ya hewa linalofanana na msimu wa sasa, ikisema itapunguza idadi ya mechi za nyumbani katika maeneo ya kaskazini katika kipindi cha kati ya Disemba na Februari. Ligi inakadiria kuwa asilimia 91 ya mechi za msimu wa 2027–28 zitaangukia ndani ya muda ule ule unaotumika kwa sasa.

Kocha wa Chicago Fire, Gregg Berhalter, alisema mabadiliko hayo yanaifanya MLS kujiweka sawa na ligi bora duniani, huku aliyekuwa nahodha wa Marekani, Clint Dempsey, akisisitiza kuwa ulinganifu wa ratiba na ligi nyingine utawafanya wachezaji kuwa “na makali zaidi” wanapokwenda kwenye timu za taifa.

Related Articles

Back to top button