Mkurugenzi TFF ataja kilichomsibu Samatta
IMEELEZWA kiwango cha Mbwana Samatta kushuka kilitokana na msongo wa mawazo aliopata kutokana na kushindwa kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya England na kutolewa kwa mkopo katika Ligi ya Uturuki.
Samatta alisajiliwa na Aston Villa ya England akitokea Genk ya Ubelgiji, lakini hakudumu England matokeo yake akapelekwa kwa mkopo Fenerbahçe ya Uturuki ambako nako hakufanya vizuri.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Oscar Mirambo alisema Samatta ndoto yake ilikuwa ni kucheza England lakini kitendo cha kusajiliwa na kushindwa kufanya vizuri kilimpa msongo wa mawazo na alipotolewa kwa mkopo ndio msongo ulizidi.
“Samatta kwa sasa amerudi kwenye kiwango chake, lakini hapa nyuma kiwango chake kilishuka kutokana na msongo wa mawazo alioupata baada ya kushindwa kumudu ushindani katika Ligi Kuu England na kutolewa kwa mkopo Uturuki,” alisema Mirambo.
Alisema kuwa na matarajio na kushindwa kufikia ni hali ambayo inawaathiri watu wengi na siyo wachezaji pekee, lakini baadaye hali hutengemaa kwa kupata waatalamu wa saikolojia.
Samatta ambaye kwa sasa anachezea Royal Antwerp Football Club ya Ubelgiji kwa mkopo, ameanza kurudisha imani kwa mashabiki baada ya kufanya vizuri timu ya taifa, Taifa Stars, katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia.
Awali mashabiki walilalanika kuwa nyota huyo hajitumi kama ilivyo kwa mwenzake Simon Msuva anayecheza Morocco.




