Ligi Kuu

Miloud  atoa tahadhari kwa wachezaji wake

DAR ES SALAAM:KOCHA  Mkuu wa Yanga, Hamdi Miloud, ameonesha wasiwasi wake juu ya kasi ya Simba katika mashindano ya kimataifa, hali iliyomlazimu kutoa tahadhari kwa wachezaji wake kuhusiana na mechi zao zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza baada ya kuonekana pengo dogo la pointi kati yao na wapinzani wao wa jadi, Hamdi amesema timu yake haina nafasi ya kufanya makosa katika hatua hii ya msimu.

Yanga inaongoza ligi kwa pointi 70 baada ya kucheza mechi 26, huku Simba ikishika nafasi ya pili kwa pointi 57 wakiwa na mechi nne mkononi.

“Hatupaswi kufanya makosa katika kila mchezo kwa sababu wapinzani wetu, Simba, wanasubiri tukosee. Tunahitaji kushinda kila mechi ili kutetea taji la ubingwa,” amesema Hamdi

Kocha huyo amesisitiza kuwa wanahitaji kujipanga kwa ajili ya mechi tatu zijazo kwa kuhakikisha wanavuna pointi zote tisa, ili kujihakikishia nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao.

“Tunatakiwa kuwa makini, kutumia kila nafasi tunayopata kutafuta ushindi na kuepuka kuwapa wapinzani wetu nafasi ya kutuvuka,” ameongeza.

Kwa hali ilivyo, ushindani kati ya vigogo hawa wawili wa soka nchini umeendelea kushika kasi, huku kila mchezo ukiwa na uzito wa kipekee kwa hatima ya ubingwa wa msimu huu.

Related Articles

Back to top button