Africa

Michuano ya Afrika: TANZANIA ina jambo lake Okt 16

KWA mara nyingine tena, wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya klabu Afrika, Oktoba 16 watakuwa kibaruani kupigania kupata matokeo ili kusonga mbele kwenye hatua zinazofuata.

Kwa bahati ni kwamba tunafika raundi ya pili ya awali tukiwa na mtaji mkubwa wa timu nne, kwa maana ya Simba, Yanga, Azam na Kipanga FC kutoka visiwani Zanzibar.

Hii imekuwa tofauti na misimu ya nyuma ilivyokuwa kwa Tanzania kusaliwa na timu mbili au moja kwenye raundi hii tena kukiwa hakuna matumaini ya kusonga mbele kwa timu hizo.

Kwa maana fupi ni kwamba msukumo ni mkubwa Tanzania kuhusu soka na kila timu inataka kufanya vizuri kuonesha umwamba wake Afrika na kwamba haikubahatisha kupata tiketi ya kushiriki michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

SIMBA SPORTS

Pamoja na yote, lakini mpaka sasa Simba ndiyo ambayo kwenye mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilifanikiwa kupata ushindi mnono wa mabao 3-1 tena ikiwa ugenini Angola dhidi ya Primiero de Agosto.

Licha ya ushindi huo, lakini tayari Simba imejinasibu kuwa bado haijamaliza na kwamba itamaliza kazi rasmi kesho ili itinge kibabe hatua ya makun di.

Wekundu hao walionesha soka safi kwenye mechi ya kwanza dhidi ya wenyeji wao na walionesha ukomavu kwa nidhamu waliyokuwa nayo dhidi ya Agosto hivyo wanahitaji hesabu chache kuondoka na ushindi Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na kuvuka kwa kishindo hatua hiyo.

Kisaikolojia hata Agosto wanaamini mambo yatakuwa magumu mno kesho kutokana na uwezo wa Simba waliouona, lakini pia ile kauli ya Simba kwamba kwa Mkapa hatoki mtu, bado imeendelea kuwa imara kila msimu timu hiyo inapoumana na wapinzani wao kwenye uwanja huo.

Kwa haraka haraka, kinachosubiriwa ni kukamilika kwa dakika 90 hizo ili Simba ianishiwe rasmi kusonga mbele, ingawa soka lina matokeo yake na linapaswa kuheshimiwa bila ya kujali umemzidi kwa kiasi gani mpinzani wako.

Simba tayari wana kumbukumbu ya kushinda mabao 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy tena ugenin, lakini ilijikuta ikifung- wa mabao 3-1 nyumbani kwenye Uwanja wa Mkapa na kutolewa kwa bao la ugenini msimu uliopita, hivyo sidhani kama watafanya kosa kama hilo.

YANGA AFRIKA

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara watakuwa na kibarua kizito kwenye mechi yao ya marudiano dhidi ya Al Hilal ya Sudan, inayotarajiwa kupigwa mjini Khartoum majira ya saa tatu usiku.

Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilishindwa kuutumia vyema Uwanja wa Mkapa na kutoka sare ya bao 1-1 na Hilal, matokeo ambayo hayana afya kuelekea mchezo huo wa kesho kwa kuwa wapo ugenini.

Yanga ilionesha kiwango kizuri kwa Mkapa, lakini mara kadhaa ilishindwa kugeuza nafasi wanazozipata kuwa mabao ambayo yangewapa mtaji mzuri kuelekea ugenini.

Hata hivyo, bado wana nafasi ya kufanya vyema kama wakiwa makini kwenye mbinu za kucheza ugenini wakihitaji bao moja ili waingie makundi kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 24 bila kufanya hivyo.

Presha ya kutoingia makundi kwa muda mrefu imekuwa ikiwasumbua Yanga kichwani na pengine kama hawataitumia vizuri iwe faida kwao, basi inaweza kuwaletea hasara kubwa na kujikuta wakiingia mwaka mwingine bila kuifikia hatua hiyo.

Yanga inapaswa kukomaa kuendeleza heshima yake licha ya kuwa hata ikifungwa na kung’olewa kwenye michuano hiyo itadondokea Kombe la Shirikisho Afrika na pengine inaweza kuwa nafasi ya pili kwao kurekebisha makosa kupitia michuano hiyo na kuionesha Afrika umwamba wake.

AZAM FC

Matajiri wa Jiji wanaoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika wenyewe wiki iliyopita wakiwa ugenini walibugizwa mabao 3-0 na Al Akhdar ya Libya. Lakini siku chache baada ya kipigo hicho waliibuka na kauli ya ‘remontada’.

Neno la Kireno linalotumika kwenye soka kama kurejea na kushinda baada ya awali kuonekana kushindwa. Azam inaamini itafanya hivyo.

MIFANO HAI

Ni timu chache duniani zimefanikiwa kufanya remontada kama vile mwaka 2019 Liverpool ilivyopindua meza dhidi ya Barcelona na kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 4-3 baada ya mechi ya kwanza kufungwa mabao 3-0 kwenye nusu fainali ya michuano ya Uefa.

Mfano mwingine hai ni pale Simba ilipofungwa mabao 4-0 na Mfulira Wanderers ya Zambia kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), Dar es Salaam kabla haijapindua meza kibabe kwa ushindi wa mabao 5-0 ugenini Zambia.

Kinachohitajika Azam kinawezekana, lakini hakiji mara kwa mara, hivyo wanapaswa kujipanga kwelikweli, kuwa na mbinu bora wakiwa nyumbani kesho Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Kocha wao, Denis Lavagne ni mzoefu wa michuano hii, mwaka jana aliifikisha fainali ya michuano hiyo, JS Kabylie ya Algeria kabla ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Raja Casablanca.

Licha ya uzoefu wake lakini pia uwepo wa wachezaji wengi wazoefu na wenye vipaji vya juu ndani ya kikosi chake kunachagiza juu ya upambanaji wao kwenye remontada. Azam wanaamini mechi haijaisha, kesho pengine inaweza kuwa nafasi yao adimu kuiaminisha Tanzania nzima juu ya hilo.

KIPANGA

Mabingwa hawa wa Kombe la FA Zanzibar nao watakuwa na shughuli ya kulinda lango lao ugenini huku wakitafuta bao litakalowapeleka hatua inayofuata ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Club Africain ya Tunisia.

Mechi ya kwanza iliyopigwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar ilimalizika kwa suluhu na kutoa mwanya kwa timu zote mbili kuanza upya kwenye mechi ya kesho ingawa hiyo haifuti faida iliyonayo Africain ambao wako nyumbani.

Kipanga imeonesha jinsi gani sio wepesi wa kutikiswa nyavu zao mara kwa mara kwani hata katika mechi ya raundi ya kwanza ya awali walitoka sare ya 2-2 dhidi ya Al Hilal Wau baada ya sare ya 1-1 kwenye mechi zote mbili kisha kuibuka na ushindi wa matuta wa mabao 4-3.

Mechi iliyopita walitembea vyema na kauli ya ‘kama hatupati bao basi na wao wasipate’ na imewasaidia kuondoa mlima mrefu ambao pengine wangelazimika kuupanda kesho tofauti na walionao sasa.

Yote kwa yote, nafasi ya Kipanga ipo wazi, kwa soka wanaloonesha na uzoefu wanaoendelea kuupata, ukichanganya na morali waliyonayo msimu huu, tusishangae kesho kukishuhudia kile ambacho hakikufikiriwa na wengi.

Related Articles

Back to top button