Mfaume:Nimeuza gari kuendesha mashindano

DAR ES SALAAM:MWANANCHI na mratibu wa michuano ya soka ya Mfaume Cup, Mfaume Mfaume, amesema ameuza gari yake ili kupata fedha za kuendesha mashindano ya vijana.
Akizungumza na SpotiLeo Mfaume amesema alifanya hayo yote baada ya kukosa udhamini na hivyo, kuomba wadau mbalimbali wakiwemo Azam kumuunga mkono kabla ya kwenda kuuza viwanja vyake kwa ajili ya kutimiza ndoto za vijana wenye vipaji wapate kuonekana.
Michuano hiyo iliyoshirikisha timu 16 imefikia hatua ya robo fainali, ambapo mechi za hatua hiyo zitachezwa Ijumaa ya wiki hii Mei 30, mwaka huu.
“Nimeweka magari yangu, najitolea mali zangu kuhakikisha michuano inaendelea. Niko tayari hata kuuza viwanja au nyumba kama ikibidi, kwa sababu najua thamani ya kuwekeza kwa vijana,” amesema bondia huyo wa ngumi za kulipwa.
Timu zilizongia hatua ya robo fainali ni Nakos, Kanu FC, Macho Macho, Nyukipori, Kagera Boys, Kimanga, Soka City ya Kimara na La Masia
Mfaume amesema: “Nilianzisha Mfaume Cup kwa lengo la kukusanya vijana pamoja, kudumisha undugu, kukuza vipaji, na pia kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza michezo nchini.
“Hii pia ni fursa ya vijana kuonekana na kupata nafasi katika timu kubwa za ndani na hata nje ya nchi,
Mfaume amesema mashindano hayo yamevutia viongozi wa timu kubwa na wachezaji maarufu kama Ibrahim Ajibu, Shaibu Ninja, na wengine waliowahi kucheza Simba na Yanga, ambao wamejitokeza kuwapa changamoto vijana na kutoa motisha kwao.
“Tunawaomba wadau wa michezo, makampuni, viongozi, na mashabiki waendelee kutuunga mkono. Ligi Kuu imemalizika, sasa ni wakati wa kushika kazi ya vijana mitaani. Kupitia Azam TV na vyombo vingine, tunaamini vipaji vya hawa vijana vitaonekana,” amesema Mfaume.