Messi, De Paul watajwa kikosi cha Argentina

BUENOS AIRES: NYOTA wa Inter Miami, Lionel Messi, na kiungo Rodrigo De Paul wamejumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Argentina kitakachocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Angola wiki ijayo.
Kocha wa Argentina, Lionel Scaloni, ametangaza majina ya wachezaji 24 kwa mchezo huo wa kirafiki utakaochezwa Novemba 14. Wakati huu, Inter Miami na Nashville FC wako kwenye hatua ya kwanza ya michuano ya mtoano ya MLS Cup, baada ya kugawana ushindi katika mechi mbili za mwanzo.
Mchezo wa tatu wa kuamua nani atasonga mbele utafanyika Jumamosi mjini Fort Lauderdale, Florida. Ikiwa Inter Miami watasonga mbele, nusu fainali ya Kanda ya Mashariki itachezwa kati ya Novemba 22 au 23.
Messi na De Paul walichezea Argentina mwezi Oktoba katika michezo ya kirafiki dhidi ya Venezuela na Puerto Rico, Messi akicheza mechi moja, huku De Paul akicheza zote mbili. Scaloni hakuwaita wachezaji wanaocheza kwenye ligi ya ndani ya Argentina, akizingatia kuwa Primera Division haitasimama wakati wa kalenda ya michezo ya kimataifa mwezi huu.

“Tulizungumza na kocha Scaloni kuhakikisha wachezaji kutoka timu za Argentina zinazoshiriki michezo ya muhimu katika mashindano ya Clausura hawajumuishwi kikosini,” alisema rais wa Shirikisho la Soka la Argentina (AFA), Claudio Tapia, kama alivyonukuliwa na ESPN jana Alhamisi.
Kipa wa Aston Villa, Emiliano Martinez, mwenye umri wa miaka 33, hakupata wito wa kujiunga na kikosi hicho kwa mechi ya kirafiki.
Messi, mshindi wa Kiatu cha Dhahabu cha MLS na kinara wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka (MVP), alijumuishwa pia kwenye orodha ya MLS Best XI msimu huu. Akiwa na mabao 29 na pasi 19 za mabao, alikosa kwa alama moja pekee kuivunja rekodi ya Carlos Vela (Goal involvements 49) iliyowekwa mwaka 2019 na anaweza kuwa mchezaji wa kwanza kushinda tuzo ya MVP mara mbili mfululizo katika historia ya ligi hiyo.




