Habari Mpya

Maudhui ya ndani ni muhimu kulinda utamaduni wa nchi

KILA Taifa duniani limekuwa likipigania utamaduni wake.

Linapoona mambo hayaendi sawa hupaza sauti kuwarudisha watu katika mstari ulionyooka. Hapa nchini, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hivi karibuni iliita wadau wa vyombo vya utangazaji, sanaa na utamaduni kuzungumzia uhamasishaji wa uzalishaji na usambazaji wa maudhui bora ya ndani.

Sababu ni baada ya kupata malalamiko kutoka kwa walaji walioshuhudia maudhui kadhaa yanayooneshwa kwenye vipindi mbalimbali vinavyorushwa kwenye vyombo hivyo vikiwa ni vya nje na hivyo kuita wadau ili kutafuta suluhu ya pamoja ya kulinda utamaduni wa ndani.

Kwa mujibu wa mmoja wa wasilicha mada kutoka TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka anasema waliandaa mkutano huo kwa makusudu ili kuhakikisha maudhui ya ndani yanakuwa yenye ubora wa kushindana na yale ya nje.

“Kama hatuna maudhui bora ya kushindana na yale ya nje, tutabaki tunapiga kelele. Hata mataifa makubwa yana kanuni na sheria zinazolinda maudhui ya ndani na wana sababu zao. Marekani na nchi za Ulaya wanatetea na kuhamasisha utengenezwaji wa vipindi vya ndani na sisi lazima tufanye hivyo.”

“Tusipofanya hivyo, vipindi vyao vitakuja kwetu na kuteka utamaduni wetu, lazima tujikwamue ili tushindane,” anasema.

Mgeni rasmi katika mkutano huo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye anasema: “Ni ukweli usiopingika kwamba sasa mabadiliko ya teknolojia ya habari na utangazaji yametupeleka kwenye dunia nyingine ambayo usambazaji wa maudhui hauna mipaka.”

Anasema kwa sasa unaweza kupokea maudhui kutoka sehemu yoyote duniani ili mradi unakifaa stahiki cha kupokelea maudhui.

Makampuni makubwa ya kimataifa yanashindana kutengeneza na kusambaza tamthiliya, cartoon za watoto, vichekesho (Comedy), miziki, makala na maudhui mengi yenye vionjo na tamaduni kutoka nchi mbalimbali.

“Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa tunatumia teknolojia iliyopo kuhakikisha kuwa na sisi tunaingia kwenye ulimwengu wa ushindani na utandawazi ambapo utavutia Watanzania na wananchi wengine walioko nje ya mipaka ili kutazama na kueneza utamaduni wetu na vilevile kuongeza pato la taifa,” anasema.

Anasema jamii imekumbwa na changamoto ya kulishwa maudhui kutoka nchi za mbali ambayo kwa kiasi kikubwa hayazingatii maadili na utamaduni wa Kitanzania na hivyo yamechangia sana kuharibu utamaduni.

“Hii imesababishwa na uhaba wa ubunifu katika utengenezaji wa maudhui ya ndani, hivyo watoa huduma ya maudhui walio wengi hawapendi kujishughulisha na kutumia ubunifu wao kuandaa vipindi badala yake hunakili maudhui mitandaoni na kuilisha jamii maudhui yasiyowafaa,” anasema.

Anasema: “Kama jamii ya Watanzania tunao utamaduni wetu, mila na desturi ambazo zinatutofautisha na jamii nyingine za kigeni.”

Waandaaji na watayarishaji wa maudhui mnayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba utamaduni wetu, mila na desturi zetu zinadumishwa na hazipotoshwi kabisa ili hata watoto wetu wanaozaliwa kizazi hadi kizazi wawe na cha kujivunia katika nchi yao kupitia vipindi ama habari wanazozipata kupitia vyombo vya habari na utangazaji.

Anasema ili kufanikisha hilo inatakiwa uwepo mkakati wa kuhakikisha jamii ya Watanzania inalishwa maudhui bora kulingana na mahitaji. Awali, Kisaka alisema nchi zote zimejiwekea asilimia 50 hadi 60 ziwe na maudhui ya ndani na kuna sheria na kanuni za uhimizaji wake katika viwango vya kimataifa.

Anasema wameamua kutetea maudhui ya ndani ili kulinda umataduni unaowatambulisha duniani. Kisaka anasema isipodhibitiwa kuna hatari kwa mfano watu watakuwa wanaangalia tamthiliya nyingi na vipindi vyenye utamaduni wa nje na matokeo yake wataiga na vizazi kwa vizazi vitaharibikiwa.

Anatolea mfano kwenye muziki wa kizazi kipya na singeli licha ya kuimba lakini maudhui yaliyoko ndani yake ni mapenzi na wengine wanaiga vitu ambavyo havifai kuanzia mavazi. Anasema zamani muziki wa dansi ulikuwa unasikilizika kutokana na maudhui yake tofauti na sasa wanapoteza utamaduni.

“Muziki unaopigwa ni wa ndani ila maudhui yaliyoko ni ya ndani, kama kuna kitu kinashawishi jamii yetu ni kile kinachoonekana. Pia, kuna katuni za watoto zenye maudhui ya nje ambazo ni hatari kwa sababu watoto wakitazama wanaiga,” anasema.

Anasema kuna vitu vyenye maudhui ya utamaduni wa nchi kama ngoma za asili lakini changamoto iliyopo hazichezwi na kuwahimiza wadau kuona uwezekano wa kuzicheza badala ya kuziona tu kwenye matukio maalumu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui, Habbi Gunze anasema wanatamani kuona mafanikio yaliyopatikana katika mpira wa Tanzania namna unavyozungumzwa kila mahali basi na kwingine kufikie hatua hiyo kwa maana ya kuona muziki, tamthiliya, vichekesho vinaoneshwa vyenye utamaduni wa Kitanzania ili uzungumzwe kila kona.

“Niwaambie kuna stori ya mafanikio ya mpira, zamani mtaani kama sio Simba na Yanga basi utasikia watu wakizungumza Man U, Arsenal lakini sasa ukipita mtaani ni mpira wa Tanzania na ni kwa sababu ya uwekezaji wa mpira wa Tanzania kutoka kwa Azam Media,” anasema.

Gunze anahoji je, asilimia 60 ya vipindi vya ndani iliyowekwa imefikiwa? Ili kusudi kiwango kiongezwe kifikie asilimia 80 na asilimia 20 iwe vipindi vya nje. Mkurugenzi wa Plus TV, Ramadhan Bukini anasema maudhui ya vipindi vingi vinaonekana kutokuwa na ubora kwa sababu ya kukosa uhuru wa kile wanachokitengeneza.

“Changamoto tunayokutana nayo ni kwamba ukitaka kuweka maudhui ya kupendeza unaambiwa hii usiweke au toa hakiruhusiwi. Unatengeneza maudhui ilimradi ipite kwa sababu unakosolewa hadi kile ulichokikusudia kinapoteza maana,” anasema.

Anasema ili kushindana na maudhui yenye ubora suala hilo liangaliwe lakini pia fedha imekuwa ni tatizo ya kufanya uwekezaji kwa kuwa wengi hupata hasara ya vitu wanavyozalisha havilipi. Itaendelea

Related Articles

Back to top button