Michezo Mingine

Mashindano ya Rugby kurindima Moshi

DAR ES SALAAM: CHAMA cha Rugby Tanzania (TRU) kimetangaza ujio wa mashindano ya kila mwaka ya kuwaenzi wachezaji waliopoteza maisha yanayoitwa Moshi Memorial 10’s Rugby Tournament.

Mashindano hayo yatafanyika Jumamosi, Oktoba 25, 2025, katika Uwanja wa Ushirika, Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa TRU Antony Dawa, mashindano hayo, yamekuwa yakifanyika kwa heshima ya kuwakumbuka wachezaji wa rugby waliotangulia mbele ya haki, sambamba na kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa saratani ya matiti.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Heshimu. Ungana. Cheza”, ikisisitiza heshima, umoja na ushindani wa michezo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa TRU, Anthony Dawa, mashindano hayo yatashirikisha timu za wanaume 10 na wanawake saba kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Dar es Salaam, Tanga na Moshi.

“Tunapenda kuwaalika wadau wote wa michezo, mashabiki na wananchi kwa ujumla kuhudhuria na kushuhudia siku kamili ya burudani na ushindani wa rugby. Ni tukio la kipekee lenye lengo la kuhamasisha afya, umoja na maendeleo ya mchezo wetu,” alisema Dawa.

Dawa alisema michuano hiyo imekuwa moja ya nguzo muhimu katika kukuza rugby nchini, ikileta pamoja timu, makocha na wadau wanaojitolea kwa ajili ya ustawi wa mchezo huo unaozidi kupanuka Tanzania.

Related Articles

Back to top button