“Mashabiki tulieni” – Maresca

LEEDS: BAADA ya kupoteza mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Leeds United kwa kufungwa mabao 3-1, kocha mkuu wa Chelsea, Enzo Maresca, amewataka baadhi ya mashabiki wanaolalamikia uamuzi wa kocha huyo wa kutowatumia baadhi ya wachezaji wake muhimu kutomuingilia kwenye majukumu yake.
Chelsea imepoteza mechi hiyo ya usiku wa Jumatano ikicheza ugenini katika uwanja wa Elland Road, na kujikuta ikiporomoka kwa nafasi moja kwenye msimamo wa EPL hiyo kutoka nafsi ya tatu hadi ya nne, kufuatia Aston Villa kushinda mechi yake.
Maresca amesema wachezaji kama Wesley Fofana, Moisés Caicedo na Reece James ni muhimu kwenye kikosi chake, lakini hawezi kuwatumia katika kila mechi, kama ambavyo mashabiki wa klabu hiyo wanataka.
Kocha huyo raia wa Italia amesema ana wachezaji wengi kwenye kikosi chake, hivyo hana ulazima wa kuwatumia kadri anavyotaka kutokana na nafasi na mechi zinazomkabili katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa mwaka.




