Mashabiki England hawataki VAR

THELUTHI mbili ya mashabiki wamesema wanapinga matumizi ya Waamuzi Wasaidizi wa Video(VAR) katika mfumo wa soka England.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji Uingereza(BBC) utafiti unaonesha asilimia 63.3 ya mashabiki hawataki VAR huku asilimia 79.1 ya watazamaji wa mechi wakisema VAR ni mbaya au mbaya sana.
Utafiti huo ni tofauti na wa mwaka 2017 uliofanywa na Chama cha Mashabiki wa Soka(FSA) kabla ya kuanza kwa VAR ambao ulionesha asilimia 74.6 ya mashabiki walipendelea matumizi ya VAR kuamua matikio tata uwanjani.
Ni asilimia 5.5 tu ya mashabiki waliosema VAR ni nzuri.
Utafiti huo wa uliofanywa na FSA umehusisha mashabiki 9645 mwezi Machi na Aprili mwaka huu.
Aidha asilimia 92 ya mashabiki waliohojiwa wamesema matukio yanachukua muda mrefu kuamuliwa huku asilimia 26.8 wakisema wanapendelea VAR kabisa au kwa kiasi fulani.
Utafiti huo pia umeonesha asilimia 80 ya mashabiki wanataka kusikia majadiliano ya sauti kati ya waamuzi wa VAR na anayechezesha mechi uwanjani.