Maresca atetea mabadiliko ya kikosi, amjibu Rooney

LONDON: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca, ametetea sera yake ya kubadilisha wachezaji mara kwa mara (Squad Rotation) baada ya kukosolewa vikali na nahodha wa zamani wa England na Manchester United, Wayne Rooney.
Rooney alisema wachezaji wakubwa wa klabu hiyo wanapaswa kuhoji maamuzi ya Maresca baada ya kufanya mabadiliko saba kwenye kikosi kilichoanza katika sare ya 2-2 dhidi ya Qarabag kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumatano.
Hiyo ilikuwa ni mechi ya tano mfululizo ambayo kocha huyo raia wa Italia amefanya angalau mabadiliko saba kwenye kikosi chake cha kwanza.

Hata hivyo, Maresca amesema kuwa nguvu ya kikosi chake inamuwezesha kubadilisha wachezaji na kuwapa nafasi wote kubaki fiti katika msimu mzima alioulinganisha na mbio ndefu ya marathon.
“Tupo katika kipindi ambacho kila mtu anaweza kusema chochote anachotaka. Tangu nimejiunga na klabu hii, nimekuwa na mtazamo wa kubadilisha wachezaji. Hakuna anayelalamika ukishinda. Ukikosa kushinda, naelewa kwamba watu hawatakubali”. – alisema Maresca akijibu ukosoaji wa Rooney.
“Nilipenda mzunguko wa wachezaji hata nilipokuwa mchezaji. Sasa hivi mpira unahitaji nguvu na kasi zaidi haiwezekani kucheza mechi 65 na kikosi kilekile.” – aliongeza
Maresca alienda mbali zaidi akisewma falsafa yake hiyo inalenga kuandaa timu vizuri kuelekea hatua za mwisho za msimu ambazo amesema timu nyingi hupoteana, kupoteza pointi na kutoka nje ya malengo waliyoanza nayo msimu.
Kocha huyo pia alimtetea beki kijana Jorrel Hato, aliyelaumiwa kwa makosa yaliyopelekea mabao yote mawili ya Qarabag mjini Baku nchini Azebaijan.

“Wakati unamzungusha mchezaji kama Andrey Santos, ambaye ni mchezaji wa kimataifa wa Brazil, Jorrel Hato, mchezaji wa kimataifa wa Uholanzi, na Estevao, mchezaji wa Brazil hapo si suala la kubadilisha tu,”
“Ni wachezaji wenye kipaji, bado vijana. Unapokuwa na vijana, lazima uwape nafasi ya kujifunza kupitia makosa. Lakini ukishindwa kushinda, lawama zinakuwa ni juu ya mabadiliko ya kikosi.”
Chelsea walio katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Premier League, watakuwa na kibarua cha kusaka pointi tatu mbele ya Wolverhampton wonderes kesho jumamosi saa 5 usiku kwa saa za Afrika Mashariki




