Maresca ashtushwa na Mudryk kuwepo Wroclaw

WROCLAW: KOCHA wa mabingwa wa UEFA Conference, Chelsea, Enzo Maresca, alionekana kushangazwa kama mtu mwingine yeyote alipoambiwa kuwa winga wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Ukraine, Mykhailo Mudryk, alionekana nchini Poland wakati ambapo Chelsea walikuwa wakijiandaa na fainali dhidi ya Real Betis jana usiku,fainali ambayo waliibuka mabingwa baada ya kuwatandika Betis 4-1.
Mudryk, ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji wakubwa waliosajiliwa na Chelsea alipowasili kwa dau la dola milioni 108 mwaka 2023, hajacheza tangu mwezi Desemba mwaka jana, ilipobainika kuwa anakabiliwa na uchunguzi kwa tuhuma za kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni.
Mpaka sasa, winga huyo wa Ukraine amekuwa kimya kwa muda mrefu, kabla ya kuzuka kwa video na picha kwenye mitandao ya kijamii zilizomuonyesha akiwa bize kupiga picha na mashabiki wa Chelsea jana Jumanne, akiwa amevalia koti lenye nembo ya klabu hiyo.
“Kusema kweli, sijui. Yuko hapa? Au anakuja? Kwani yuko hapa? Nimefurahi kama Misha (Mudryk) yupo hapa. Sijui, nina furaha tu kama Misha yupo hapa,” alisema Maresca huku akitazama huku na huko kwa mshangao alipoulizwa katika mkutano wake na wanahabari ikiwa amemuona winga huyo mjini Wroclaw kuelekea mchezo huo wa fainali.
Mudryk hajachapisha chochote kwenye mitandao yake ya kijamii tangu taarifa kuhusu kisa chake cha dawa zilizopigwa marufuku michezoni, mnamo Desemba mwaka jana, alipokiri kuwa “kitu kilichopigwa marufuku”—ambacho hakikutajwa—kilipatikana kwenye sampuli aliyotoa.




